Biashara ya kikatili ya watoto Nigeria ambapo wanawake hutekwa, hupewa uja uzito na watoto wao kuuzwa

Katika uvamizi wa mwisho katika kiwanda hicho maafis wa polisi walifanikiwa kuwakamata watoto wanne na wanawake 19

Walikwenda kutafuta ajira na kuishia kutekwa , kubakwa na watoto wao kuuzwa.

Katika sehemu ya mwisho ya biashara ya ulanguzi wa binadamu nchini Nigeria, polisi waliwaachilia huru wanawake 19 waliokuwa wametekwa na kuwanusuru watoto wanne waliopatikana katika kilichotajwa kuwa 'kiwanda cha watoto' mjini Lagos.

Wanawake hao walidanganywa na kuahidiwa kazi kwa lengo la kupata uja uzito na baadaye kuwauza watoto, kulingana na mamlaka.

Bado haijulikani ni wanawake gani waliopatikana na wananuzi wa watoto hao ni akina nani, lakini mamlaka nchini Nigeria ilifichua kwamba wanawake hao huuza watoto wa kike kwa takriban $ 830 na wavulana kwa $ 1,400.

Wakati wa operesheni , wanawake wawili waliokuwa wauguzi bila ya mafunzo yanayohitajika walikamatwa ijapokuwa mshukiwa mkuu alitoroka.

Wanawake wote na watoto wote waliopatikana wamewekwa katika nyumba ya kubadilisha tabia.

Wanawake hao walisafiri hadi lagos baada ya kuwaahidi kazi

Tangu 2006 ripoti ya shirika la Umoja wa mataifa kuhusu watoto UNESCO ilielezea kwamba uwepo viwanda vya watoto nchini Nigeria, ambapo vituo kama hivyo vimeenea katika taifa hilo hutokana na umasikini na ukosefu wa udhibiti kutoka kwa utawala.

Ripoti hiyo vilevile inasema kwamba baadhi ya wanawake wanaotumika katika biashara hiyo hujitolea bila kujua hatma yao kwa lengo la kuimarika kiuchumi .

Udanganyifu

Wanawake wanaookolewa huwa na kati ya umnri wa miaka 15 hadi 28 na hupelekwa Lagos , Mji mkuu nchini Nigeria wakiahidiwa kupata ajira.

Lakini wanapowasili huzuiliwa na kubakwa.

Changamoto za kiuchumi nchini Nigeria zilisababisha wanawake wengi kudanganywa

''Mwanamke alinichukua katika kituo cha basi na kunileta hapa siku iliofuata, niliitwa na mkuu wetu ambaye aliniambia kwamba sitaondoka katika nyumba hiyo hadi mwaka ujao'', alinukuliwa mmoja ya waliookolewa akizungumnza na gazeti la Nigeria The Vanguard. ''Kufikia sasa , nimelalala na wanaume saba tofauti'' .

''Waliniambia kwamba baada ya kujifungua nitalipwa vizuri'' , mwanamke huyo aliendelea.

Mwathiriwa mwengine aliambia BBC jinsi alivyotekwa kinyume na matakwa yake na hakuruhusiwa kuondoka alipogundua kwamba mwanawe atauzwa.

Mwengine alisema simu yake na fedha zilichukuliwa na baadaye kuambiwa hawezi kupata matibabu licha ya hali yake.

Ramani ya Nigeria

Tatizo la kiafya

"Tatizo la viwanda vya watoto nchini Nigeria ni kwamba limeenea na limekuwepo kwa muda fulani.

Kisa cha Lagos ni cha kusikitisha sana , lakini sio tatizo jipya, alisema Debbie Ariyo, mwanzilishi wa kipindi cha BBC Today, kutoka Muungano wa Afrika dhidi ya unyanyasaji wa watoto AFRUCA.

Kulingana na Ariyo, swala la maeneo kama hayo kusheheni ni kutokana na sababu tatu.

Sababu ya kwanza ni umasikini katika maeneo ambayo wanawake hawa wadogo hutoka, la pili ni kwamba , wanawake hawa hukataliwa baada ya kupata uja uzito swala linalowashinikiza kuondoka makwao ili kutafuta msaada.

Ya tatu na muhimu zaidi kulingana na Ariyo, ukosefu wa nguzo thabiti katika taifa hilo ambazo huzuia, kudhibiti na kuzuia kuchipuka kwa biashara kama hizo.

Zaidi ya watoto 160 wameokolewa.

Mnamo mwezi Aprili 2018, wasichana 100 na wavulana 62 waliokolewa na maafisa wa polisi kutoka katika kiwanda kimoja cha watoto mbali na nyumba mbili za watoto mayatima mjini Lagos.

Watoto huuzwa kwa thamani ya dola 1000 ya Marekani

Wakati huo, baadhi ya watoto hao wakubwa na wachanga walionyesha ishara za kunyanyaswa kingono.

Mwaka 2013, vijana 17 na watoto 11 waliokolewa kutoka katika nyumba moja jimbo la Imo, katika eneo la kusini mashariki mwa taifa hilo.

Baadye watoto hao walisema kwamba wamebakwa na mtu mmoja.

Ni mfano tu wa tatizo kubwa ambalo Utawala wa Nigeria haujui jinsi ya kulikabili.