Mtoto Aastha Arora: Raia wa bilioni moja wa India yuko wapi?

Mtoto Aastha Arora

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Aastha Arora muda mfupi baada ya kuzaliwa kwake

Aastha Arora alikaribishwa duniani kwa shangwe nyingi.

Ndani ya saa chache baada ya kuzaliwa kwake saa 05:05 tarehe 10 Mei 2000 katika hospitali ya Safdarjung ya Delhi, mtoto huyo mchanga aliorodheshwa kama "raia bilioni moja wa India".

Mawaziri wa serikali walipigwa picha wakiwa wamembeba mtoto huyo mchanga aliyekuwa amefukwa blanketi laini la waridi.

Kuzaliwa kwa mtoto Aastha kuliifanya India kujiunga na China, nchi pekee iliyo na zaidi ya watu bilioni moja.

Katika hafla iliyofanyika kusherehekea hatua hiyo muhimu, mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu India Micheal Vlassoff alimtaja Aastha kama mtoto "wa kipekee sana".

Maafisa pia walisema kwamba kuzaliwa kwake kuliibua suala la kutafakari upya njia za kudhibiti idadi ya watu inyoongezeka kwa kasi nchini India.

Lakini sherehe za kuzaliwa kwa mtoto huyo ziligonga vichwa vya habari duniani na, kwa siku kadhaa baada ya hapo, waandishi wa habari walipiga foleni kuelekea nyumbani kwao huko Najafgarh, eneo lenye watu wa tabaka la kati waliosongamana kusini magharibi mwa Delhi.

Mimi pia nilikuwa sehemu ya waandishi wa BBC waliyozuri nyumbani kwao kumuona mtu mashuhuri mdogo zaidi wa India na kuzungumza na mama yake, Anjana Arora.

Zaidi ya miongo miwili baadaye, niliwatembelea tena ili kujua “mtoto huyo wa pekee” alikuwa wapi sasa na jinsi alivyokuwa akiendelea.

Aastha Arora akiwa na picha yake akiwa mtoto
Maelezo ya picha, Aastha Arora hivi karibuni alipata kazi yake ya kwanza

Kijana mwenye umri wa miaka 22 ambaye alinifungulia mlango siku ya Jumapili hivi majuzi asubuhi aliniambia kwamba aliacha kujihisi maalum zamani na kudai kwamba ahadi nyingi ambazo wanasiasa walitoa wakati wa kuzaliwa kwake hazikutimizwa.

Sababu iliyomfanya anione Jumapili ni kwa sababu ndiyo siku pekee ya kutoka kazini - hivi majuzi alianza kufanya kazi kama nesi katika hospitali ya kibinafsi.

"Nilitamani kusomea sayansi na kuwa daktari, lakini wazazi wangu hawakuwa na uwezo wa kunipeleka katika shule ya kibinafsi hivyo nililazimika kukubaliana na kufanya mazoezi ya uuguzi," ananiambia.

Aastha ananionyesha kabrasha la vijisehemu vya magazeti vilivyotungwa na wazazi wake kuhusu maisha yake - ni kutokana na haya ambapo alijifunza kuhusu hali ya kuzaliwa kwake na fadhaa inayoambatana nayo.

Umakini uliendelea kwa muda baada ya kuzaliwa kwake. Kulingana na ripoti moja, alialikwa kuzindua tovuti, iliyoanzishwa kwa pamoja na wizara ya afya ya India na UNFPA, alipokuwa na umri wa miezi 11.

Wiki moja baada ya siku yake ya kuzaliwa, siku moja akiwa na familia yake katika jiji la Ajmer ilifunikwa na chapisho la ndani ambalo liliandika kuhusu jinsi "alifurahia kurarua vitabu vya kiada vya kaka yake mwenye umri wa miaka mitano na kazi za nyumbani".

Aastha anasema yeye mwenyewe alianza kufahamu hadhi yake maalum alipoanza shule.

"Pengine nilikuwa na umri wa miaka minne au mitano niliposikia neno mtoto wa bilioni kwa mara ya kwanza katika siku ya idadi ya watu ya Umoja wa Mataifa, wakati wanahabari walipotua shuleni kwangu," anasema.

"Kwa mtoto lilikuwa jambo kubwa kuonekana kwenye TV na nilipenda umakini wake."

 Aastha alijifunza kuhusu hali ya kuzaliwa kwake kutoka kwa vijisehemu vya magazeti

Kuangaziwa katika vyombo vya habari pia kulitafsiriwa katika manufaa fulani yanayoonekana kwake.

Baba yake, ambaye alifanya kazi kama mfanyabiashara katika duka, alipata zaidi ya dola 50 kwa mwezi na alikuwa akijitahidi kulipa karo ya shule ya watoto wake wawili.

“Kila mwaka waandishi wa habari waliponitembelea kufanya habari juu yangu, ilimaanisha pia kutangazwa bure kwa shule, hivyo waliniondolea ada baada ya darasa la pili,” anasema.

Huko shuleni, Aastha alistawi - alikuwa mzuri katika taaluma, alishiriki katika mijadala na maonyesho ya densi, na aliteuliwa kuwa mkuu wa kundi la shule yake.

Alipokuwa na umri wa miaka 16, shule ilimtunuku "tuzo la mtu mwenye neema".

Lakini licha ya alama zake bora, hali mbaya ya kifedha ya familia ilimlazimu kubadili shule ya serikali katika kiwango cha 11.

"Sikuwa na furaha sana katika shule mpya na ilionekana katika darasa langu," anasema, akiongeza kuwa ulikuwa mwisho wa ndoto yake ya kuwa daktari.

Ijapokuwa wazazi wake walikuwa maskini, mama yake anasema kwamba kwa muda baada ya kuzaliwa kwa Aastha, kila ndoto ilionekana kufikiwa.

 Aastha akiwa na wazazi wake na kaka yake
Maelezo ya picha, Aastha akiwa na wazazi wake na kaka yake

Familia yake haina nyaraka za kuthibitisha madai hayo, lakini inasema kwamba Sumitra Mahajan - wakati huo waziri wa maendeleo ya wanawake na watoto - alikuwa amemuahidi binti yao "elimu ya bure, huduma ya afya bila malipo na njia ya reli ya bure" alipokuwa akiwatembelea hospitalini.

Bi Arora anasema kwamba katika ziara nyingine nyumbani kwao miezi michache baadaye akiwa na mbunge wa eneo hilo wakati huo Sahib Singh Verma, walikuwa wamewahakikishia kwamba wangesaidia kumtafutia babake kazi serikalini.

"Tulijaribu kuwasiliana na ofisi yake mara nyingi baada ya hapo lakini tuliambiwa kila mara kuwa hayupo," aliongeza.

Familia hiyo inasema msaada pekee wa kifedha waliopokea ulitoka kwa UNFPA ambayo ilianzisha mfuko wa rupee 200,000 ($2,425; £2,118) ambazo familia inaweza kutumia kwa elimu ya chuo kikuu cha Aastha mara tu alipokuwa na umri wa miaka 18.

Mfuko huo, ambao ulikua rupee 700,000, ulisaidia kulipia sehemu ya kozi yake ya uuguzi.

Bw Verma alifariki mnamo 2007, lakini nilimpigia simu Bi Mahajan, ambaye alistaafu kutoka kwa siasa mwaka 2019 baada ya kuhudumu kama Spika wa bunge la India, ili kumuuliza kuhusu madai ya familia hii.

Bi Mahajan alisema hakumbuki ni ahadi gani - ikiwa zipo - zilitolewa kwa familia isipokuwa hazina iliyoahidiwa na UNFPA.

"Niliitembelea familia kama waziri na haikuwa kwa nafasi yangu binafsi," alisema.

"Nilikuwa waziri kwa muda mfupi na baada ya hapo ijapokuwa nilikuwa Delhi, nilielekeza juhudi zangu katika siasa.

Lakini familia hiyo haikuwahi kuwasiliana nami. Kama wangeniandikia barua, bila shaka ningesaidia," aliniambia na kuongeza kuwa "hata leo wakiniomba nitajaribu kuwasaidia".

Sherehe ya kuzaliwa kwa mtoto wa mabilioni pia ilikusudiwa kuwa wakati wa kutafakari kwa kina, ili kutoa ujumbe kwa wananchi kwamba ukuaji huu wa kasi wa idadi ya watu usio endelevu, kwamba idadi ya watu inayongezeka itaifanya serikali kukabiliwa na changamoto ya kutoa huduma za msingi na kuinua viwango vya maisha.

India ni nchi ya pili kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu duniani

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, India inatabiriwa kuipiku China kama nchi yenye watu wengi zaidi duniani mwaka 2023

Katika miaka ya hivi karibuni, Aastha pia ametilia maanani suala hili - kwenye mikutano ya hadhara ameelezea idadi kubwa ya watu wa India kama "tatizo".

"India lazima ifanye kitu kudhibiti idadi ya watu," aliniambia, akiongeza kuwa "ni upendeleo wetu wa kitamaduni kwa wana ndio umetufikisha hapa".

"Watu wanaendelea kupata watoto wa kike hadi wapate mtoto wa kiume kwa sababu wanaamini kwamba mtoto wa kiume ataendeleza kizazi chao.''

Serikali, anasema, lazima ifanye kazi kubadili mawazo. Mnamo 2000, wakati Aastha alizaliwa, makadirio ya serikali yalionyesha kuwa India inaweza kuipiku China na kuwa nchi yenye watu wengi zaididuniani ifikapo 2045.

Mnamo Julai, UN ilisema itafanyika mapema mwaka ujao, na idadi ya watu wa India kufikia bilioni 1.4.

"Tayari kuna ushindani mkubwa kwa kila kitu, watu wengi sana wanapigania nafasi sawa shuleni na vyuoni na kwa kazi sawa," anasema Aastha.

"Nilikuwa mtoto wa bilioni moja, hivi karibuni tunaweza kupata mtoto wa bilioni mbili," anaongeza. "Natumai hatutawahi kufikia hatua hiyo muhimu."