Mbinu za kufanya mtoto wako asiangalie picha za ngono

Chanzo cha picha, Getty Images
Watoto ambao ni wanafunzi mara nyingi hulalamika kwamba utendaji wao au akili zao zinashuka.
Wazazi wa mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 15 walimpeleka kwa mtaalamu wa saikolojia, baada ya kubaini kwamba mtoto wao alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani hadi alipofika darasa la sita, lakini sasa hazingatii masomo yake.
Wakati daktari alipoongea na mtoto huyo peke yake, alifanikiwa kugundua tatizo. Alitoa ushauri kwa wazazi wa mtoto ambao ulisaidia kuboresha utendaji wake shuleni.
Wazazi wa mtoto huyo waligundua hapo awali kwamba mtoto alikuwa na simu ya mkononi kwa muda mrefu usiku na mchana.
Mtoto alimwambia daktari kwamba alikua akienda chumbani kwake na kufunga mlango, na simu yake ilikuwa imezuiwa kwa neno la siri. "Tulipomuuliza maswali, alisema anazungumza na marafiki na alikasirika."
Mtaalamu wa saikolojia na mtaalamu wa masuala ya ngono, Dkt. Ashok, aligundua tatizo kuwa mtoto alikuwa akikwepa masomo kutokana na kutazama picha za ngono na alikua akipendelea kukaa peke yake,na kujitenga na watu.
Hili ni suala linalolalamikiwa na wazazi katika nchi nyingi duniani.
Hivi karibuni, kesi ilifunguliwa dhidi ya mwanaume katika jimbo la Kerala nchini India kwa kutazama ponografia katika mazingira ya umma.
Wakati wa kesi hii, ilisemwa kwamba kutazama ponografia si uhalifu nchini India, lakini ikiwa watoto wangeanza kufanya hivyo wakiwa na umri mdogo, madhara yake yanakuwa kwa muda mrefu.
Mahakama ilisema kwamba wazazi wanapaswa kufahamu hatari ya kuwapa watoto simu na wanapaswa kuwahimiza kutazama video za kielimu mbele yao au kucheza michezo ya video inayohusu watoto.
Mbinu ambazo wazazi wanaweza kutumia kuzuia watoto kutazama picha za ngono

Chanzo cha picha, Getty Images
Dkt. Ashok anasema kwamba watoto sasa wanakumbana zaidi wa maudhui ya ngono kutokana na teknolojia kuliko ilivyokuwa zamani. "Pia kuna picha na maudhui kama hayo kwenye mitandao ya kijamii."
Anasema kwamba tangu janga la Corona, simu na vifaa vya kielektroniki vimechukua nafasi ya walimu na imekuwa vigumu wazazi na walimu kugundua vifaa hivi vinapotumiwa na watoto.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, wazazi hawapaswi kuchukua hatua haraka kutokana na taharuki ya kugundua kwamba mtoto wao anatazama ponografia.
"Haisaidii pia kuwakasirikia watoto kwa sababu ni rahisi zaidi kufanya hivyo kutaongeza shauku yao kufuatilia maudhui kama hayo."
Anashauri kwamba "njia bora ni kuwaelezea watoto kwa upole na kwa utulivu na kuwafanya waelewe matatizo yanayoweza kutokea kutokana na kutazama ponografia."
"Ukikasirika, utafanya hali kuwa mbaya zaidi, siyo kutatua tatizo."
Wanasema kwamba watoto kwa kawaida hucheza mbali na wazazi wao, jambo ambalo ni la kawaida, lakini "ikiwa wazazi wataona kwamba watoto wao wako peke yao na wamezingatia simu zao, basi ni muhimu wazungumze na mtoto."
"Waulize ikiwa kuna tatizo lolote, wawapatie muda, wawaambie jinsi gani wazazi wao wanavyowapenda."
Kubadilisha mazingira na kula pamoja na watoto kunaimarisha uhusiano kati ya wazazi na watoto.
Dkt. Ashok anasema kwamba uhusiano huu ni muhimu kwa sababu ni wakati huo tu watoto wataweza kuwaambia wazazi wao kile kinachotatiza fikra zao.
Hatua nyingine muhimu ni kwamba baada ya umri wa miaka 11, watoto huanza kuonyesha shauku ya kujifunza kuhusu ngono kwa njia ya asili.
"Hiyo ndiyo maana ni muhimu kwa wazazi kuwaambia watoto wao kuhusu hili ili wasipoteze mwelekeo wao," anasema Dkt. Ashok.
Anasema kwamba baada ya umri wa miaka 11, watoto wanapaswa kufundishwa kuhusu uvutaji sigara, unywaji pombe na ngono. "Kwa njia hiyo watapata ufahamu."
"Kadri watoto wanavyokua, maswali kuhusu mabadiliko ya kimwili huibuka vichwani mwao, na ikiwa hawatapata majibu thabiti au maelezo, wanaweza kuvutiwa na ponografia," anasema.
Anaongeza umuhimu wa elimu ya ngono shuleni, akisema kwamba kushindwa kutekeleza hatua hizi pia ndiko kunavyopelekea watoto kuvutiwa na dawa za kulevya.