Samia Suluhu Hassan aingia kwenye orodha ya watu wenye ushawishi mkubwa Duniani miongoni mwa Waislamu

.

Chanzo cha picha, SAMIA SULUHU/TWITTER

Maelezo ya picha, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Taasisi ya Kifalme Al-Bayat ya Jordan kwa ajili ya Kiislamu yaani The Royal Al Al-Bayat Institute for Islamic Thought (RABIIT) imetoa orodha ya watu 500 wenye ushawishi wa Kiislam kutoka duniani kote kwa mwaka 2023.

Taasisi ya Kifalme ya Al-Bayat kwa ajili ya Uislamu, ni asasi ya Kiislamu na ina makao yake makuu huko Amman, mji mkuu wa Jordan.

Ingawa ushawishi wa 50 bora unatawala vitengo vingi na hauwezi kuegemea kitengo kimoja au kingine, inaweza tu kuwa busara kuiweka katika vitengo vya jumla zaidi, kulingana na ripoti hiyo.

Katika 50 Bora yaliongezwa majina ya Waheshimiwa na kuchaguliwa kwa kuzingatia makundi matatu ya jumla ambayo ni:

1. Watawala na Wanasiasa

2. Wasomi na Wahubiri

3. Wanao jihusisha na masuala ya Kijamii, Vyombo vya Habari, Sayansi, Sanaa, Utamaduni na Michezo.

Katika orodha hiyo, Mfalme Salman bin Abdul-Aziz Al-Saud wa Saudi Arabia yuko nambari moja, Ayatollah Ali Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Iran nambari mbili na Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani, mtawala wa Qatar nambari tatu.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan yuko nambari nne, Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed bin Zayed Al-Nahyan namba nane na Mtawala wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman namba 10.

Joko Widodo, Rais wa Indonesia, nchi yenye waislamu wengi zaidi duniani, ni nambari 15 katika orodha hii.

Orodha hiyo pia ilijuisha wengine kutoka barani Afrika akiwemo rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye ameorodheshwa kuwa namba 38.

Rais Samia Suluhu Hassan

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Samia Suluhu Hassan ni Rais wa Tanzania aliyeingia madarakani baada ya kutokea kwa kifo cha mtangulizi wake John Magufuli Machi 2021.

Ameweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo wa juu zaidi nchini Tanzania.

Pia anakuwa rais wa pili wa Tanzania kutokea Zanzibar, wa kwanza akiwa Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyeliongoza taifa hilo kwa miaka 10 kutoka mwaka 1985 hadi 1995.

Aina ya kuchukua hatamu kwa Samia kumekuja kwa mara ya kwanza nchini Tanzania, yaani kwa rais kufariki akiwa madarakani na makamu wake kuchukua nafasi.

Kwa Watanzania wengi, jina la Samia Hassan Suluhu lilipata umaarufu zaidi wakati alipoteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba lililoteuliwa mwaka 2014.

Tanzania ilikuwa inaelekea kutengeneza Katiba mpya - baada ya kukamilika kwa kazi ya kukusanya maoni ya wananchi kupitia Tume ya Jaji Warioba na Mama Samia alikuwa amepewa jukumu la kuongoza mchakato huo kupitia Bunge la Katiba.

Kwa sababu bunge lile lilikuwa likionyeshwa moja kwa moja kupitia vituo mbalimbali vya runinga na Watanzania wengi wakiwa na kiu kubwa ya kujua nini kinaendelea - sura ya Samia ilianza kuzoeleka kwenye macho ya wengi na uwezo wa kuongoza ukionekana dhahiri.

Katika duru za kisiasa bungeni wakati ule, Samia alikuwa akifahamika kwa uwezo wa kuonyesha utulivu - hata katika nyakati ambazo hali ya hewa katika bunge hilo ikiwa imechafuka na pia kuzungumza na wote.

Muundo wa bunge hilo ulitaka viongozi wake wa juu watoke katika pande mbili za muungano na kwa vile mwenyekiti wa bunge hilo alikuwa ni hayati Samuel Sitta kutoka Tanzania Bara, nafasi ya Makamu Mwenyekiti iliangukia kwa Mzanzibari Samia.

Hata hivyo, wengi hawakutarajia kwamba angetangazwa na aliyekuwa mgombea urais wa chama cha mapinduzi mwaka 2015, John Magufuli, kuwa mgombea mwenza wake kwenye uchaguzi huo.

Ingawa wakati huo tayari alikuwa na uzoefu wa uwaziri wa takribani miaka 15; kujumlisha na uzoefu wake huo katika Bunge la Katiba- si watu wengi walimwona yeye kama mmoja wa watu wanaoweza kupewa wadhifa huo.

Wakati CCM iliposhinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 - unaotajwa kuwa mgumu kuliko yote kwa chama hicho tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini - Samia aliweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo tangu kuanzishwa kwa taifa la Tanzania.

Rais Muhammadu Buhari Rais wa Nigeria

.

Chanzo cha picha, AFP

Rais Muhammadu Buhari alishinda muhula wake wa pili kama Rais wa Nigeria mnamo Februari 2019, akimshinda mpinzani wake kwa zaidi ya kura milioni tatu.

Katika orodha ya Shirika la RABIIT ameshikilia namba 17.

Katika miaka hii, alipata umaarufu kwa vita vyake vyote dhidi ya ufisadi na utovu wa nidhamu, sifa ambayo ameihifadhi tangu wakati huo.

Rais Buhari aligombea kama mgombea mkuu wa upinzani katika chaguzi za urais za 2003, 2007 na 2011, zote zikiishia kwa kushindwa, kabla ya kushinda 2015.

Anachukuliwa kuwa kigogo na Waislamu wa kaskazini mwa Nigeria lakini anafurahia heshima ya taifa kutokana na msimamo wake kuhusu ufisadi.

Kati ya malengo yake aliyoyapa kipaumbele ni kushinda kundi la wapiganaji la Boko Haram.

Vitendo vya Boko Haram mara kwa mara vimesababisha hasira ya kimataifa, na Rais huyo ameonyesha kujitolea hadharani kusitisha mashambulizi ya kigaidi.

Tarehe 6 Mei 2017, serikali ya Buhari ilifanikisha kuachiliwa kwa wasichana 82 kati ya 276 waliotekwa nyara mwaka 2014, kwa mabadilishano ya viongozi watano wa Boko Haram.

Rais Buhari alikutana na wasichana wa Chibok walioachiliwa kabla ya kuondoka kwenda London.

Rais Buhari alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Shirika la Kitaifa la Petroli la Nigeria (NNPC) na alikuwa mpangaji mkuu wa ujenzi wa bohari 20 za mafuta nchini Nigeria, mradi unaohusisha zaidi ya kilomita 3200 za mabomba.

Viwanda vya kusafisha mafuta vya Warri na Kaduna vilijengwa chini ya uongozi wake.

Mnamo 2020 maandamano dhidi ya madai ya ukatili wa polisi wa kitengo maalum cha Jeshi la Polisi la Nigeria Kikosi cha Kupambana na Ujambazi (SARS) yalizuka huko Lagos na miji mingine mikubwa.

Siku moja baada ya waandamanaji kutangaza madai yao Rais Buhari alitangaza kuvunjwa kwa kikosi cha SARS na kuahidi ‘’mageuzi makubwa ya polisi’’.

Maandamano hayo yalisababisha kuuawa kwa waandamanaji kadhaa.

Mohamed Salah

,

Chanzo cha picha, Getty Images

Mohamed Salah ni mchezaji wa soka wa Misri na maarufu duniani ambaye katika orodha hiyo ameshikilia namba 39.

Alizaliwa Juni 15, 1992 na alichaguliwa kupitia kitengo cha ushawishi wa Watu Mashuhuri na Michezo.

Salah alianza soka lake katika Ligi Kuu ya Misri mwaka 2010 kabla ya kuhamia Uswizi, Uingereza, Italia na kisha kurejea Uingereza tena.

Salah alifurahia msimu wenye mafanikio zaidi katika maisha yake ya soka akiwa na Liverpool FC 2017/18.

Alivunja rekodi nyingi na kushinda tuzo nyingi.

Pia aliisaidia Misri kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Msimu wa mwaka  2018/19 alipata mafanikio zaidi kwa Liverpool FC kuwa washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Uingereza, na kutawazwa Mabingwa wa Ulaya wa 2019 na Mabingwa wa Vilabu vya Dunia.

Msimu wa 2019/20 ulifisha kikomo muda wa kusubiri kwa miaka 30 kwa Liverpool kuwa mabingwa wa ligi ya Uingereza tena.

Tabia yake ya urafiki na adabu imemletea mashabiki wengi kote ulimwenguni, na hakuna zaidi kuliko katika nchi yake ya asili ya Misri ambapo ametoa michango mbalimbali ya hisani.

Ana wafuasi zaidi ya milioni 217 kwenye mitandao ya kijamii.

Akitoa orodha hiyo kwa mwaka 2023, Rabbit ameandika katika ripoti yake, "Kuna Waislamu bilioni 1.94 duniani hivi sasa.

Idadi hii ni theluthi ya idadi ya watu wote duniani.

Waislamu hawa ni raia wa nchi husika, lakini pia wana uhusiano wa aina yake na jamii ya Kiislamu duniani kote.

Wafahamu waliorodheshwa katika nambari nne za mwanzo

1 . Mfalme Salman bin Abdul-Aziz Al-sad

.

Chanzo cha picha, AFP

Shirika la RABIIT limemuweka Mfalme Salman katika orodha ya Waislamu wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani kwa mwaka 2023.

Mfalme Salman ni mfalme wa saba wa Saudi Arabia aliingia uongozini mnamo Mwezi Januari 2015.

Shirika la RABIIT limeandika kuwa Mfalme Salman ana ushawishi mkubwa katika nchi za Kiarabu.

Maka na Madina ni miji miwili mitakatifu nchini Saudi Arabia, ambapo mamilioni ya Waislamu hutembelea kila mwaka. Saudi Arabia pia ina jukumu kuu duniani katika usambazaji wa mafuta.

Mbali na hilo, Waislamu wa kawaida huingia Saudi Arabia kila mwaka kwa ajili ya Umrah.

2. Ayatollah Ali Khamenei

.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Ayatollah Ali Khamenei

Ayatollah Ali Khamenei amewekwa nambari mbili kwenye orodha hii.

Khamenei ni kiongozi mkuu wa Irani.

Ayatollah Khamenei ni mtu wa pili mpaka sasa kuchaguliwa kwenye wadhifa huo.

3. Emir Sheikh Tamin bin Hamad Al-Thani

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani

Sheikh Tamin bin Hamad Al-Thani alikuwa Emir wa Qatar akiwa na umri wa miaka 33.

Pato la Taifa kwa kila mtu nchini Qatar ni $63,505 na kwa mantiki hiyo ni nchi tajiri zaidi duniani.

Qatar ni kinara wa kuuza gesi na ina hifadhi ya tatu kwa ukubwa wa gesi duniani.

Thani alikuwa mfalme mwaka 2003.

Shirika la RABIIT limeandika kwamba mama yake Sheikha Moza bado ana nguvu sana na anachukuliwa kuwa na jukumu muhimu katika utawala wa Qatar.

Sheikh Tamin amesoma kutoka shule binafsi nchini Uingereza.

4. Recep Tayyip Erdogan

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Recep Tayyip Ardoan alikuwa Rais wa Uturuki kwa miaka 11.

Erdogan alishinda uchaguzi wa 2002, 2007 na 2011 kwa kura nyingi.

Erdogan alichaguliwa kuwa rais mwaka wa 2014.

Mnamo 2018, pia alipata muhula wa pili wa Rais.

Uturuki ilibadilika kwa njia nyingi chini ya utawala wa Erdogan.

Ardogan alikua meya wa kwanza wa kihafidhina wa Kiislamu wa Istanbul mnamo 1994.

Baada ya kuwa Waziri Mkuu wa Uturuki kwa mara ya kwanza mnamo 2002, Ardogan alisema katika mahojiano na New York Times, ‘’Mimi ni Muislamu kabla ya chochote. Kama Muislamu, ninafuata dini yangu. Nina wajibu kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hiyo, nimekuwa mimi.Ninajaribu kutimiza wajibu huo.’’