'Ningekatwa kichwa': Uasi wa wanajihadi waongezeka nchini Msumbiji

Chanzo cha picha, AFP
"Iwapo [wanajihadi] wangegundua mimi ni afisa wa serikali, wangenikata kichwa," Tomas Langa, mtumishi wa serikali kaskazini mwa Msumbiji, aliiambia BBC.
Anahisi alikuwa na bahati ya kutoroka. Tumebadilisha jina lake kwa ajili ya usalama wake.
Akiwa ameshtushwa na milio ya risasi alfajiri ya Mei 10, Bw Langa alichungulia nje ya dirisha lake na kuona watu wanne wenye silaha wamesimama nje ya nyumba yake katika mji wa Macomia, jimbo lililokumbwa na waasi la Cabo Delgado.
Aliogopa sana na kukimbilia mashambani, ambako alijificha kwa siku tatu akiishi kwenye shamba la mihogo.
"Nilikuwa na bahati walinitukana tu nilipokuwa nikikimbia," alisema.
Wapiganaji wanaohusishwa na kundi la Islamic State (IS) walilenga majengo ya serikali na wafanyakazi wake katika mji huo kabla ya kupora maduka na maghala.
Watu hao wenye silaha walizingira eneo hilo kwa siku mbili, na hivyo kujenga mazingira ya hofu na machafuko.
Wanajihadi walivamia kituo cha matibabu kinachoendeshwa na shirika la misaada la Médecins Sans Frontières (MSF), na kukamata magari na vifaa vya matibabu.
MSF ilisema haikuwa na budi ila kuwahamisha wafanyikazi na kusitisha shughuli zake huko Macomia.
Alfane Silva, baba wa watoto watano, aliambia BBC kwamba alizuiliwa na kuhojiwa na watu wanane wenye silaha. Pia naye, hili si jina lake halisi.
"Walikuwa wamevalia mavazi ya kijeshi na wamebeba silaha nzito," alisema.
"Waliniambia nikimbie msituni la sivyo wataniua ikiwa ningebaki mjini."
Bw Silva alisema ilichukua siku mbili kwa vikosi vya serikali kufika, lakini kufikia wakati huo wanamgambo walikuwa tayari wameondoka.
Zaidi ya watu 700 walitoroka mapigano hayo ya hivi punde huko Macomia, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM).
Wale waliosalia nyuma, kama Bw Silva na Bw Langa, wameachwa bila vifaa vya matibabu, hawana umeme, na wanaishi kwa hofu ya kushambuliwa tena.
Ilikuwa ni kupungua kwa ghasia hizo zilizozuka hivi punde zaidi huku vikosi vya usalama, vikisaidiwa na wanajeshi kutoka mataifa jirani, vikionekana kudhibiti hali hiyo.
Lakini sasa, wengi wa wanajeshi hao wanaondolewa.

Chanzo cha picha, Reuters
Ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) wenye wanajeshi wapatao 2,000 kutoka nchi nane, umesema utaondoa vikosi vyake kutoka Msumbiji ifikapo tarehe 15 Julai, na kutoongeza muda wake wa miaka mitatu.
Wataalamu wa usalama wa kikanda wameonya kuwa huenda hilo likatokea mapema mno, kwani eneo hilo bado halijatulia.
Botswana na Lesotho tayari zimewaondoa wanajeshi wao, huku Angola na Namibia zikiwa katika harakati za kuondoka.
Hata hivyo, Tanzania, ambayo inapakana na nchi hiyo upande wa kaskazini, itadumisha wanajeshi 300, linaripoti gazeti la kibinafsi la Zambeze, lenye makao yake makuu katika mji mkuu wa Msumbiji, Maputo.
Dastan Kweka, mtaalamu wa masuala ya utawala nchini Tanzania, aliambia BBC kwamba mamlaka inatarajia usalama katika eneo hilo kuendelea kuzorota.
Afrika Kusini, ambayo kwa sasa inachangia zaidi ya wanajeshi 1,000 katika juhudi za kulinda amani, imesema itaweka wanajeshi wake nchini Msumbiji hadi mwisho wa 2024, lakini sio kama sehemu ya ujumbe wa Sadc.
Kwa upande mwingine, Rwanda ambayo si sehemu ya Sadc lakini imeiunga mkono Msumbiji, ilitangaza kutuma wanajeshi 2,000 wa ziada nchini humo.
Msemaji wa jeshi la Rwanda Brig-Jenerali Ronald Rwivanga aliambia BBC kwamba walikuwa "wakiimarisha" nguvu zao. Uamuzi huo hauhusiani na kujiondoa kwa Sadc au mashambulizi ya hivi karibuni, alisema.
Rwanda ilipotuma wanajeshi wake 1,000 wa kwanza mwaka 2021, ilisema inaunga mkono juhudi za kurejesha mamlaka ya serikali ya Msumbiji huko Cabo Delgado.
Hii ilifuatia kutiwa saini kwa mikataba kadhaa baina ya nchi hizo mbili mwaka 2018.
Wanajeshi wa ziada wa Rwanda watasaidia kuziba mapengo yaliyoachwa na wanajeshi wa Sadc kaskazini mwa Msumbiji.
Meron Elias, mchambuzi wa Afrika Mashariki na Kusini wa shirika la Crisis Group, alisema ujumbe wa Sadc nchini Msumbiji unakabiliwa na matatizo ya kifedha, ukitegemea sana michango ya nchi wanachama ili kuendelea.
Alisema muungano wa kikanda badala yake, umeelekeza zaidi juhudi zake katika kuleta utulivu kuliko na hali ya hatari huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mnamo Disemba 2023, Sadc ilituma wanajeshi wake DR Congo kusaidia serikali kupambana na maelfu ya vikundi vya waasi ambao wanasumbua mashariki mwa nchi.
Shambulio la Kiislamu kaskazini mwa Msumbiji

Kundi la al-Shabab lenye uhusiano na IS nchini Msumbiji - ambalo halina uhusiano na kundi lenye jina sawa na hilo nchini Somalia - limekuwa likifanya kazi huko Cabo Delgado tangu 2017.
Waasi wake wameua mamia ya watu, kuchoma miji na vijiji na kufanya jamii kutoroka makazi yao.
Wamekuwa wakipigania kudhibiti eneo hilo ambalo lina utajiri wa gesi asilia na madini kama vile hidrokaboni, grafiti na rubi.
Mnamo Julai 2021, kampuni kubwa ya nishati ya Ufaransa ya Total Energies ililazimika kusimamisha mradi wake wa gesi asilia iliyosafishwa wa $20bn (£16bn) kufuatia shambulio la kushangaza katika mji wa Palma.
Baada ya kutumwa kwa wanajeshi wa Sadc na Rwanda mwaka huo huo, mashirika ya misaada na serikali yaliripoti kuwa usalama umeimarishwa katika baadhi ya maeneo na maisha ya kawaida yalikuwa yakirejea taratibu.
Kwa bahati mbaya, maendeleo haya yalikuwa ya muda mfupi.
Tangu Desemba 2023 mashambulizi yamekuwa yakiongezeka tena.
Zaidi ya watu 110,000 wamelazimika kutoroka makazi yao, kulingana na IOM.
Tomas Queface, mtafiti katika tovuti ya Cabo Ligado ya Msumbiji inayofuatilia ghasia hizo, alisema wanamgambo hao walifanikiwa kuishikilia Macomia kwa siku mbili kwa kusajili wapiganaji zaidi wakiwemo watoto.
Ripoti ya kikundi cha kampeni cha Human Rights Watch ilitaja watu wawili kutoka kwa familia moja ambao walimwona mpwa wao mwenye umri wa miaka 13 akifanya uporaji pamoja na wanajihadi wakati wa shambulio hilo.
Majirani wa kaskazini mwa Msumbiji wanatazama kile kinachoendelea kwa woga.
Mnamo mwaka wa 2020, wanajihadi walishambulia vijiji vya mpakani mwa Tanzania, na kuua karibu watu 25, kupora maduka na kuchoma nyumba.
Tangu wakati huo, Tanzania imeimarisha usalama kwa kuweka amri ya kutotoka nje katika baadhi ya vijiji vya mpakani, kuongeza doria na kuzuia harakati kati ya nchi hizo mbili.
Bw Kweka alisema ingawa mkakati huu umefaulu umekuwa ghali. Bajeti ya ulinzi ya Tanzania imeongezeka kwa 10% kila mwaka tangu 2021.
Wakati huo huo, kuna wasiwasi kwamba kama uasi wa Cabo Delgado utaendelea zaidi, nchi nyingine jirani, kama Malawi, zinaweza kuathirika ikiwa waasi watavuka mpaka, kulingana na mchambuzi Meron Elias.
Alisema kuna ushahidi wa ushirikiano wa kikanda unaoendelea kati ya al-Shabab nchini Msumbiji na vikosi vya waasi wa Allied Defence Forces, tawi la IS linalofanya kazi nchini DR Congo na sehemu za Uganda - ingawa kiwango cha ushirikiano hakiko wazi.
Wataalamu wa usalama wa kikanda wanasema kwamba vikosi vya jeshi vya Msumbiji vinaweza kupata ushindi wa kijeshi ikiwa vitaimarishwa zaidi, na huu sio wakati wa kuwaondoa wanajeshi kutoka nchi za kigeni.
Lakini suluhu pekee la muda mrefu ni kushughulikia changamoto za kijamii na kiuchumi zinazopatikana kaskazini mwa nchi, ambako viwango vya maisha ni vya chini kuliko kusini, na kuchochea malalamiko ya ubaguzi, ambayo yanatumiwa na wanajihadi.