Kuanzia Dos Santos hadi Mugabe - mizozo ya mazishi ya viongozi wa zamani Afrika

Chanzo cha picha, EPA
Hii ni kuhusu mizozo inayozuka kuhusu maeneo ya mwisho ya kupumzisha miili ya viongozi wa Afrika lakini haimaanishi kuwa kutakuwa na utata kuhusu mahali pa kupumzika kila rais wa barani Afrika anapofariki .
Mwandishi wa BBC amefuatilia mzozo wa mahali pa kuzikwa Rais wa zamani wa Angola José Eduardo dos Santos aliyefariki nchini Uhispania tarehe 8 Julai.
Rais wa sasa João Lourenço na mke wa nne wa Dos Santos wanataka kuuleta mwili wake nyumbani kwa ajili ya mazishi ya kitaifa na maziko katika kaburi kubwa la kifahari.
Lakini binti yake Welwitschia "Tchizé" dos Santos anataka mazishi ya faragha na eneo binafsi la kaburi nchini Uhispania, ambapo watoto wake wanaweza kutembelea.
Anasema anaungwa mkono na baadhi ya ndugu zake ambao wanakabiliwa na shutuma za ufisadi nchini Angola na wanaweza kukamatwa iwapo watarejea.
Mmoja wa watoto wa Dos Santos anasema serikali haina wajibu wa kikatiba kuchukua jukumu la mazishi ya baba yake na uamuzi lazima uwe wa familia.
Hoja hiyo kuhusu haki za serikali kwa mwili wa rais aliyefariki sio kitu kigeni hutokea mara kwa mara.
Huko nyuma mwaka 2019 kulikuwa na hali kama hiyo nchini Zimbabwe wakati Robert Mugabe alipofariki miaka miwili mbele baada ya miaka yake 37 madarakani kumalizwa na Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa, kwa kuungwa mkono na jeshi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kila mtu alifikiri kuwa Mugabe angezikwa katika eneo la mashujaa la Acre katika mji mkuu, Harare. Kwani, eneo hilo ilikuwa limejengwa na yeye Mugabe na ndiye alisimamia kuzikwa kwa wenzake wengi wa zamani katika harakati za ukombozi, akiwemo Sally, mke wake wa kwanza.
Mnangagwa alianza kujenga kaburi la kuvutia la kiongozi huyo wa uhuru, lakini familia ya Mugabe isingepata chochote, baada ya kufukuzwa mamlakani na kusalitiwa na wafuasi wake.
Walibishana, mwili huo ulikuwa wa familia na baada ya mabishano ya wiki kadhaa, familia ilishinda na Mugabe, shujaa asiyepingika wa mapambano ya ukombozi wa Zimbabwe, akazikwa kijijini kwao, bila wawakilishi wowote rasmi wa serikali kuwepo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hata Kenneth Kaunda, rais wa kwanza wa Zambia baada ya uhuru na mkuu wa amani, hakuweza kupata mahali pa kupumzishwa bila mzozo kuzuka mwaka jana.
Kulingana na familia, alitaka kuzikwa karibu na mkewe na sio katika eneo rasmi ambalo serikali ilikuwa imeweka.
Kwa wakati huo, familia haikusisitiza haki zao na "KK" kama marehemu Kaunda alivyojulikana kwa upendo alipumzishwa katika makaburi ya makumbusho ya taifa ya Embassy Memorial Park katika mji mkuu, Lusaka.
Kutoka uhamishoni hadi heshima
Mizozo hii kuhusu miili ya viongozi waliofariki si mipya. Ghana pia imewahi kutokea matukio kama hayo.
Kiongozi wa kwanza - Kwame Nkrumah alifariki alipokuwa akipatiwa matibabu huko Bucharest nchini Romania.
Alizikwa kwa mara ya kwanza huko Conakry nchini Guinea, ambako alikuwa akiishi uhamishoni.
Mwili wake baadaye uliletwa Ghana. Kulikuwa na shughuli ya kiserikali ya kuaga mwili wake katika mji mkuu wa Accra na alizikwa kijijini kwao Nkroful.
Miaka kadhaa baadaye, kaburi kubwa linalofaa la lilijengwa huko Accra na mwili uliletwa na kuzikwa hapo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kila baada ya muda, kunakuwa na manung'uniko kutoka kwa familia yake huko Nkroful wakiomba mwili wake urudishwe kwao.
Mwaka 2012, Rais John Evans Atta-Mills alifariki akiwa madarakani na kutafuta mahali pa kupumzisha mwili wake halikuwa suala la moja kwa moja.
Baadhi ya wanafamilia walitaka mwili huo upelekwe kijijini kwao kwa mazishi, mabishano hayo hayakupata mvuto mkubwa wakati huo.
Mahali pa kwanza ambapo serikali ilichimba kaburi kwa ajili ya kumwombea paliachwa kwa sababu haakufaa. Hatimaye alizikwa kwenye bustani.
Maelewano basi yalikuwa kwamba bustani hiyo ingetumika kama mahali pa kuwazika marais wote wa Ghana.
Tangu wakati huo, rais mwingine wa zamani Jerry Rawlings alifariki.

Chanzo cha picha, Getty Images
Sio tu kwamba hakupelekwa mahali ambapo Rais Atta-Mills alipumzishwa, lakini familia yake katika kijiji cha kwao ilishutumu serikali kwa kumiliki mwili huo.
Alizikwa kwenye makaburi ya kijeshi huko Accra, kwa heshima kamili ya kijeshi.
Wiki chache zilizopita, Ghana iliadhimisha kumbukumbu ya miaka 10 ya kifo cha Atta-Mills.
Bado kuna mabishano juu ya kaburi lake, ni nani anayepaswa kulitunza na nini kinapaswa kuandikwa juu yake.
Pia kuna wanafamilia wake ambao bado wanataka mwili huo ufukuliwe katika bustani hiyo inayofadhiliwa na serikali huko Accra na kupelekwa kijijini kwake kuzikwa.
Kwa hivyo, moja ya hatari ya kuwa rais katika Afrika ni kwamba hakutakuwa na mahali pa kuupumzisha mwili wako unapoaga dunia.