Kwanini wanasayansi wanajiandaa kwa janga lingine la afya?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Angela Henshall
- Nafasi, BBC World Service
- Akiripoti kutoka London
Wanasayansi wamepaza sauti juu ya kile wanachohofia kinaweza kuwa janga linalofuata - ugonjwa ambao tayari umekuwa ukiharibu maelfu ya mashamba kwa miezi kadhaa.
Watafiti wanaochunguza jinsi magonjwa yanavyoenea wanaonya kwamba huenda hata tusitambue kwamba Marekani imepita kikomo cha homa ya ndege kuwa janga la binadamu, kutokana na ufuatiliaji usiokuwa na matokeo ya uhakika.
Ili kuipa jina sahihi, aina ya Homa ya Mafua ya Ndege, H5N1, sasa imefikia kila bara isipokuwa Australasia. Imegunduliwa hata katika penguins za Antarctic, na kwa ngamia huko Mashariki ya Kati.
Ugonjwa huo sasa unapatikana kwa ndege wa mwituni na mamalia katika majimbo yote 50 ya Marekani, na umesabaakutoka mashamba ya kuku na kuambukiza zaidi ya mifugo 1,000 ya ng'ombe wa maziwa, kulingana na Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA). watu 70 wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya ugonjwa huo na mtu mmoja amefariki.
Fursa muhimu ya kudhibiti virusi vya ugonjwa huo ilikwama wakati utawala wa Rais Trump na wa mtangulizi wake Joe Biden zilipopokezana madaraka, kulingana na mtaalam wa magonjwa ya ya kuambukiza Dk Caitlin Rivers, profesa msaidizi katika Chuo cha Afya ya Umma chaa Johns Hopkins Bloomberg. Kwa mfano, majimbo tofauti yamepuuza sheria tofauti zinazohusiana na usafirishaji wa mifugo.
"[Homa ya ndege] si tatizo la muda - kulikuwa na hofu kya kuzuka kwa ugonjwa huo. Sasa ni wazi kwamba unastahili kudhibitiwa na ili kufanya hilo lazima mikakati ya ugunduzi wa virusi kuimarishwa. Kipaumbele kwa sasa ni ugunduzi. Kuwabaini watu walioambukizwa, hali yao ilivyobadilika- hilo ndio tishio kubwa."
Je, homa ya ndege ndio janga linalofuata?
Wataalamu wa magonjwa wana wasiwasi ulimwenguni kote - sio Marekani pekee - ambayo huenda haijajiandaa vya kutosha kukabiliana na mlipuko wa hopa ya ndege.
"Ikiwa hatutachukua tahadhari kama inavyohitajika virusi hivi vitaendelea kusambaaa kwa mamalia wengine, na hali itakuwa mbaya ikiwa mlipuko wa sasa ya wa virusi miongoni mwa wanyama wa Marekani huenda ukachochea janga lingine," Profesa wa Tiba katika Chuo Kikuu cha Toronto, Kamran Khan alisema.
"Tunajua kihistoria, H5N1 imekuwa virusi hatari sana kwa watu," aliongeza.
Tangu Novemba 2003, zaidi ya maambukizo 700 ya virusi vya H5N1 yameripotiwa kwa Shirika la Afya Duniani, haswa kutoka nchi 15. Miongoni mwao, Indonesia, Vietnam na Misri ziliripoti idadi kubwa zaidi ya watu waliombukizwa.
Kwa hivyo homa ya ndege sio jambo geni, lakini wanasayansi sasa wana wasiwasi kwa sababu kuu tatu: kwanza, idadi kubwa ya spishi za mamalia walioambukizwa (takribani 70 kulingana na UN) kutoka kwa shamba na wafanyikazi wa shamba, hadi maeneo ya wanyamapori na wanyama wa nyumbani. Pili, kasi ya kusambaa kwa virusi miongoni mwa ng'ombe wa maziwa, ambao wanatangamana kwa karibu zaidi na wanadamu.
Kuna hali ya sintofahamu inayosababishwa na utawala mpya wa Trump: wafanyakazi katika mashirika mengi ya serikali ambao ni wataalam wa magonjwa ya kuambukiza wamefutwa kazi, na kusababisha mpango wa kupima homa ya ndege kusitishwa katika hali ambayo imewafanya baadhi ya wafanyakazi wa mashambani wa kigeni wanasita kufanyiwa uchunguzi kwa hofu ya kufukuzwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, binadamu wanapata homa ya ndege?
Kuna uwezekano wa janga la ugonjwa wa zoonotic - ambao unasambaa kutoka kwa wanyama kwenda kwa wanadamu.
Mnamo Aprili, kulikuwa na milipuko 59 iliyoripotiwa kuathiri kuku na ndege wengine 44 kutokana na maambukizi ya mamalia katika eneo la Amerika, Asia na Ulaya, kulingana na Shirika la Afya la Wanyama Duniani (WOAH).
Tangu Desemba 2024, pia kumekuwa na maambukizi ya virusi vya H5N1 miongoni mwa wanadamu nchini Marekani, Uingereza, India, Mexico, Cambodia na Vietnam.

Chanzo cha picha, Anadolu/Getty Images
Kwa miongo kadhaa, homa ya ndege ilikuwa hasa virusi vya ndege ambayo ilisababisha matatizo ambayo hayakuwaathiri watu vile, lakini sasa inavamia sana spishi zingine za ndege kwa muda mfupi zaidi.
Dk Rivers anaonya kuwa virusi hivi visipodhibitiwa, hali inaweza kuwa mbaya.
Ndege hawatambui mpaka wa kimataifa na wanasayansi wana wasiwasi kwamba tunapoingia katika msimu wa wa kiangazi ambapo ndege wengi wanahama kutoka eneo moj ahadi lingine hali ya maambukizi itaongezeka bela shaka.

Chanzo cha picha, China Photos / Stringer/ Getty Images
Je kuna chanjo ya homa ya ndege?
Kuwachanja wanyama wa nyumbani ni suala ambalo limezua utata. Wakulima ambao wanalazimika kufuga aina tofauti ya ndege wanatakiwa kuwachanja wote - kuanzia bukini hadi kuku - lakini hii sio rahisi..
Ni vigumu kufikia kiwango kinachohitajiki cha chanjo kutokana na sababu moja au nyingine - dawa kuisha madukani, hali ambayo huenda ikiwafanya wakulima kutowapa chanjo wanyama wao wote. Pia kuna suala la muitikio wa chanjo. Kuna visa ambapo wakulima wenyewe hawataki kuwachanja wanyama wao, anaelezea Dk Munir Iqbal, mkuu wa Ugonjwa wa homa ya ndege katika Taasisi ya Pirbright nchini Uingereza.
"Ufaransa kwa mfano, imekuwa ikiwachanja bata na viwango vya maambukizi vimedhibitiwa kwa kiasi kikubwa nchini humo. Imedhoofisha mzunguko wa maambukizi lakini hiyo ni kwa misingi ya kikanda," anasema.
Umoja wa Ulaya unaandaa miongozo itakayowezesha kila taifa kuchanja, lakini hata ndege aliyechanjwa bado anaweza kusambaza virusi hivyo kwa baadhi ya ndege wa mwituni.
Serikali ya Marekani kwa muda mrefu imekuwa ikikataa chanjo ya kuku, ikihofia kwamba chanjo unaweza kuathiri mzunguko wa chakula wa Marekani katika hali ambayo inaweza kuhatarisha bidhaa za wanyama kukupigwa marufuku kusafirishwa nje ya nchi, lakini Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA) hivi majuzi imetoa idhini ya masharti ya chanjo iliyoboreshwa ili kukinga kuku dhidi ya virusi vya H5N1.

Vipi kuhusu kuwachanja wanadamu?
Mashirika ya serikali nchini Marekani na mataifa mengine yamekuwa yakihifadhi mamilioni ya dozi za chanjo ya homa ya ndege kwa ajili ya binadamu.
"[Hizi] zitatumika tu katika mazingira hatarishi, kwa hivyo kwa wafanyikazi wanaotangamana kwa ukaribu na wanyama," Dk Khan alisema.

"Ikiwa hii itakuwa janga la virusi vya influenza, basi aina hiyo ya virusi itatumika kutengeneza chanjo mpya na kuizalisha kwa kiwango kikubwa," anaongeza.
Uzalishaji huu utahitaji muda, lakini hifadhi ya sasa itakuwa na nakisi.
"Tuna baadhi ya dawa ambayo haiendani ana ile inayopendekezwa, lakini inapaswa kutoa kiwango fulani cha kinga katika hatua za awali za janga."
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi