Watu wawili wathibitishwa kuwa na virusi vya Mpox Tanzania

Chanzo cha picha, getty
Mamlaka za afya nchini Tanzania zimethibitisha kuwepo kwa visa viwili vya ugonjwa wa Mpox baada ya watu wawili kugundulika kuwa na maambukizi hayo.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya imeeleza kuwa wagonjwa hao walibainika baada ya kuonyesha dalili za ugonjwa huo, ikiwemo vipele usoni, mikononi, miguuni, na sehemu nyingine za mwili, pamoja na homa, maumivu ya kichwa, vidonda kooni, na maumivu ya viungo kama misuli na mgongo.
Licha ya kutofafaua zaidi kuhusu wagonjwa hao na mahali walipo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, mmoja wa waathirika ni dereva wa magari ya mizigo anayesafiri nje ya nchi.
Uchunguzi wa maabara uliofanyika Machi 9 ulithibitisha maambukizi hayo. Kwa sasa, mamlaka zinaendelea na uchunguzi na ufuatiliaji wa visa vingine ili kuhakikisha wale waliopata maambukizi wanapata matibabu sahihi.
Ugonjwa wa Mpox unanasababishwa na virusi vinavyopatikana kwa wanyama wa jamii ya nyani, na huambukizwa kwa kugusana moja kwa moja na wanyama wenye maambukizi au kupitia maji maji yao. Pia, ugonjwa huu unaweza kusambaa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kupitia kugusana na majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa au kushiriki mavazi na vifaa vya matumizi binafsi.
Pamoja na kuthibitisha uwepo wa ugonjwa huo nchini, serikali ya Tanzania imewahimiza wananchi kuchukua tahadhari kwa kufuata kanuni za kujikinga, ikiwa ni pamoja na kuepuka kugusana na wanyama au mtu mwenye maambukizi.
Hata hivyo, wananchi wametakiwa kuendelea na shughuli zao za kila siku kama kawaida huku wakizingatia miongozo ya afya ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo.
Shirika la afya duniani (WHO) limeupa uzito ugonjwa huo na limekuwa likifanya kazi na nchi zilizoathirika na washirika wake kudhibiti mlipuko wake.
Ugonjwa huo ulitangazwa kuwa hali ya dharura kwa afya ya umma kimataifa mnamo Agosti 14, 2024, baada ya kuongezeka kwa visa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kuenea katika nchi jirani.
Lakini mlipuko wa ugonjwa huo duniani ulianza Mei 2022 na umekuwa ukiendelea hadi leo. Katika miezi ya hivi karibuni, visa vimekuwa vikiongezeka zaidi huo DRC na kutishia kuenea kwa maambukizi katika nchi jirani, ikiwemo Tanzania.
Aina mpya ya virusi, iitwayo Clade Ib, inasababisha milipuko katika maeneo ambayo hayakuathiriwa hapo awali nchini humo na imeenea katika nchi ambazo hazijaripoti mpox hapo awali.