Sherehe ya harusi ya kifahari ilioanza mwezi Machi inaelekea tamati

cd

Chanzo cha picha, reuters

Maelezo ya picha, Baada ya miezi kadhaa ya sherehe, harusi ya Ambani inaelekea kukamilika
  • Author, Zoya Mateen & Meryl Sebastian
  • Nafasi, BBC

Kiasi gani ni kupita kiasi? Hilo ndilo swali ambalo wengi nchini India wanauliza huku sherehe za harusi ya mtoto wa kiume wa tajiri mkubwa zaidi barani Asia, ikiingia awamu ya mwisho.

Sherehe hizo zinatarajiwa kufikia kilele wikendi hii wakati Anant Ambani, mtoto wa mwisho wa mwenyekiti wa Reliance Industries, Mukesh Ambani, atakapofunga ndoa na Radhika Merchant, binti wa mfanyabiashara mkubwa wa maduka ya dawa Viren na Shaila Merchant.

Kumekuwa na miezi minne ya matukio ya kifahari kuelekea harusi yenyewe. Mavazi ya kupendeza, vito vya kuvutia, mapambo adimu, watu maarufu kutoka India na kimataifa.

"Harusi ya kifalme sio fupi," anasema mwandishi na mwanasafu wa Shobhaa De.

“Wahindi siku zote wanapenda urembo na maonyesho," anasema, akiongeza kuwa "kiwango [cha harusi] kinalingana na utajiri wa Ambani.”

Pia unaweza kusoma

Utajiri wao

c

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Wazazi Neeta na Mukesh Ambani wameifanya harusi hiyo kuwa kubwa

Wakiwa na himaya kubwa ya biashara - kuanzia mafuta, mawasiliano ya simu, kemikali, teknolojia na chakula - Ambanis wapo kila sehemu nchini India na maisha yao ni mada ya kuvutia kwa umma.

Utajiri wa Ambani unakadiriwa kuwa dola za kimarekani bilioni 115. Anant, mwenye umri wa miaka 29, anashikilia wadhifa katika bodi ya wakurugenzi ya Reliance Industries.

Ambani pamoja na mfanyabiashara mwenzake wa India Gautam Adani, inaelezwa kuwa wako karibu na serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi, na vyama vya upinzani vikiishutumu serikali kwa kupendelea familia hizo mbili - shutuma ambazo serikali na wafanyabiashara hao wanakanusha.

Ukubwa wa sherehe

F

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Kama sehemu ya sherehe, familia iliandaa harusi kubwa kwa wanandoa wasio na uwezo

Mwezi Machi Ambani aliandaa karamu ya siku tatu ya kabla ya harusi ya mwanawe. Sherehe hiyo ilifanyika katika mji wa nyumbani wa familia hiyo wa Jamnagar katika jimbo la magharibi la Gujarat, ambalo pia ni eneo la kiwanda cha kusafisha mafuta cha Ambani – kiwanda kikubwa zaidi duniani.

Wageni wapatao 1,200 walihudhuria, akiwemo Mark Zuckerberg wa Meta na Bill Gates wa Microsoft.

Sherehe ilianza kwa chakula cha jioni katika jumba la kifakhari lililojengwa kwa ajili ya hafla hiyo. Muundo wa jumba hilo unafanana na Palm House, lililoko Brooklyn Botanic Garden, Marekani.

Sherehe hiyo ilifuatiwa na onyesho la Rihanna na video za mtandaoni zilionyesha familia ya Ambani ikijumuika na mwimbaji huyo jukwaani.

Wapishi mashuhuri walipika vyakula 2,000, vyenye asili ya nchi tofauti, wageni waliwekwa katika mahema ya kifahari, wakiwa na wapambaji na wanamitindo wakiwahudumia.

Pia kulikuwa na mwongozo wa kurasa 10 juu ya kanuni za mavazi kwa ajili ya matukio hayo, ambayo yalijumuisha mavazi kwa ajili ya kutembelea hifadhi ya wanyama inayomilikiwa na familia hiyo, ikifuatiwa na sherehe katika ukumbi mkubwa ambao ni sehemu ya makazi yao ya kifahari.

Bibi harusi mtarajiwa alivalia mavazi yaliyotengenezwa kwa hariri, vito na mavazi mengine ya gharama.

Bwana harusi alivalia mavazi ya Dolce & Gabbana na saa ya mkononi ya Richard Mille, yenye thamani ya takribani dola za kimarekani milioni 1.5m. Video ya mtandaoni ya Zuckerberg na mkewe Priscilla Chan wakitazama saa hiyo ilisambaa nchini India.

Magazeti na tovuti zilinasa utajiri na matukio haya ya kuvutia, yaliyohudhuriwa na watu wakubwa kutoka kote ulimwenguni.

DFDF

Chanzo cha picha, REUTER

Maelezo ya picha, Shah Rukh Khan amehudhuria hafla za kabla ya harusi

Serikali ya India iliufanya uwanja mdogo wa ndege wa jiji hilo kuwa uwanja wa ndege wa kimataifa, ikaongeza wafanyakazi wake na kupeleka wanajeshi wa ardhini na wanajeshi wa angani kuhudumia familia.

Usiku wa mwisho wa tukio la siku tatu, ambalo lilimalizika kwa mvua ya fashifashi na mwanga wa taa za kumeremeta, zikiashiaria kile sasa kitakachofuata.

DS

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Majina makubwa ya Bollywood, hapa ndipo mahali pake

Sherehe ikaendelea: Mwezi Juni, wanandoa na wageni walianza safari ya kabla ya harusi nje ya nchi. Sherehe hiyo iliyojumuisha mastaa wakubwa wa Bollywood, ilianza safari ya kifahari kwenye ufuo wa bahari ya Tyrrhenian nchini Italia, hadi Bahari ya Ufaransa.

Walisimama Roma, Portofino, Genoa na Cannes kwa tafrija za usiku sana ambazo ziliripotiwa kuleta malalamiko kutoka kwa wenyeji. Fauka ya hayo, wasanii wakubwa walikuwa wakitumbuiza.

Wiki hii, sherehe nyingine ya harusi hiyo ilianza kwenye uwanja wa nyumbani wa familia, Mumbai, kwa onyesho la Justin Bieber.

Video yake akiimba pembeni ya jukwaa huku bibi harusi na marafiki zake wakiimba pamoja imetazamwa mara milioni 38.

Kiwango cha sherehe hizo kinaonyesha kuwa hakuna kitu kisichoweza kufikiwa na familia hiyo. Na kuna uvumi kwamba Adele huenda akatumbuiza kwenye harusi yenyewe wikendi hii.

Bila shaka, India si ngeni kwa utamaduni wa harusi kubwa za kifakhari - nchi ndiyo inatumia pesa nyingi zaidi kwa sherehe za ndoa baada ya Marekani.

Watoto wengine wa Ambani pia wamefanya sherehe za kifahari za kabla ya harusi. Hillary Clinton na John Kerry walikuwa miongoni mwa waliohudhuria tafrija ya kabla ya harusi ya Isha Ambani mwaka 2018, na Beyoncé alitumbuiza.

Mwaka mmoja baadaye, tafrija ya kabla ya harusi ya Akash Ambani ilitumbuizwa na msanii Coldplay. Lakini harusi hii ya sasa, imepita harusi zote.

Maandalizi ya miaka miwili

C

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Mkurugenzi Mtendaji wa Meta Mark Zuckerberg alikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria sherehe za kabla ya harusi mwezi Machi

Ashwini Arya, mmiliki wa kampuni ambayo imesimamia harusi katika nchi 14, anasema "hii ni harusi ambayo maandalizi yake yanahitaji angalau miaka miwili, safari nyingi za kwenda na kurudi, vibali baada ya vibali kutoka nchi kadhaa, pamoja na utaratibu wa kupanga usalama na usafiri kwa baadhi ya watu wakubwa duniani."

Akina Ambani hawajafichua ni kiasi gani harusi hii inawagharimu lakini inakadiria kuwa "tayari wametumia kati ya rupia bilioni 11 na 13, sawa na dola za kimarekani 132 - 156.

Inaelezwa kuwa Rihanna alilipwa dola za kimarekani milioni 7 kwa kutumbuiza wake, huku ikielezwa kuwa Bieber amelipwa dola za kimarekani miliono 10.

Pesa pia zilitolewa kwa kujenga mahekalu 14 ndani ya jumba kubwa la Jamnagar ili kuonyesha urithi wa kitamaduni wa India na kutoa mandhari ya harusi hiyo. Kama sehemu ya sherehe hizo, Ambani waliandaa harusi kubwa kwa wanandoa 50 wasiojiweza.

Inasemekana familia imefanya harusi kubwa kwa sababu watoto wote wa Ambani wameolewa na kuoa, hii itakuwa harusi yao ya mwisho.

Lakini kuna ukosoaji wa umma wa sherehe hizo - hasa hasira juu ya trafiki katika jiji ambalo tayari linakabiliwa na msongamano wa magari na mafuriko ya monsuni.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi