Je, Upweke una athari gani kiafya?

A person walking alone in a beach

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kujitenga kwa makusudi kunaweza kuwa na faida kwa afya yako ya akili.
  • Author, ออนเดร เบียร์นาธ
  • Nafasi, บีบีซี เวิลด์ เซอร์วิส
  • Twitter,

Dk Andrea Wickfield, mkurugenzi wa kituo cha kushughulikia Upweke katika Chuo Kikuu cha Sheffield Hallam huko Uingereza, anasema "upweke ni hali ya huzuni na hisia ya kutoridhika inayotokana na kujihisi uko peke yako kinyume na vile unavyohitaji.

Wataalamu wengi wanakubali kwamba upweke hutokea unapohisi ubora wa mahusiano yako binafsi na watu wengine yako chini kuliko vile unavyotamani yawe.

Upweke sio suala la kuwa peke yako tu, hata wakati ukiwa huko peke yao, unaweza kuhisi upweke katikati ya umati wa watu, anasema Dk. Wickfield. Kuwa na hisia kwamba huna uhusiano wa kutosha na jamii kunaweza kusababisha mabadiliko ya hisia, na kupelekea upweke.

Lakini kuna tofauti kati ya upweke na kujitenga. Profesa Dk Nguyen Thuy Vi, Mhadhiri wa Saikolojia na Mtafiti Mwandamizi katika Maabara ya Solitude Studies katika Chuo Kikuu cha Durham nchini Uingereza, anaeleza, kujitenga ni pale mtu anapojitenga kimwili na watu, bila kushirikiana na mtu yeyote au bila kutumia mitandao ya kijamii.

Kujitenga kwa hiari kwa muda kunaweza kuwa na manufaa kwa afya yako ya akili. Kutokana na wingi wa simu, barua pepe, na mwingiliano na watu, hutufanya kuwa na muda mchache wa kuwa peke yetu.

Pia unaweza kusoma

Upweke unavyoharibu Afya Yako

A man seating on a  sofa looking in the direction of the window

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Utafiti umegundua upweke unahusishwa na shida ya akili, kupoteza kumbukumbu, wasiwasi, na hatari ya kifo.

Kujihisi mpweke ni kitu kibaya kiafya. Utafiti wa hivi karibuni wa Chuo Kikuu cha Cambridge umegundua, hisia za upweke zinahusishwa na hatari kubwa ya ugonjwa wa moyo. Pia huongeza hatari ya kiharusi, kisukari cha aina ya 2, na maambukizi.

Dk Wigfield anasema wanasayansi wamepata ushahidi kwamba upweke husababisha shida ya akili, unyogovu na wasiwasi, na huongeza hatari ya kifo kutokana na mambo hayo.

Sababu hasa ya uhusiano huu bado haijulikani, lakini madaktari wanakisia upweke unaweza kusababisha msongo wa mawazo wa ndani. Upweke wa muda mrefu unaunyima ubongo vichocheo vinavyochochea michakato ya fikra, na hilo linaweza kuzidisha matatizo ya afya ya akili.

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linasema mtu mmoja mzima kati ya watu wazima wanne ametengwa na jamii, na makadirio yanasema kati ya 5% na 15% ya vijana hukumbwa na upweke.

Makundi fulani ya watu yako katika hatari zaidi ya kukumbwa na upweke, ikiwa ni pamoja na wahamiaji, jamii za wachache, wakimbizi, watu wa LGBTQ, walezi na watu wenye magonjwa sugu.

Jinsi ya kuushinda upweke

A woman looking through a window steamed up with condensation

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wakati wa janga la COVID 19 watu wengi walihisi upweke.

Utafiti unasema, kujitolea kufanya shughuli za kijamii ni njia nzuri ya kuzuia upweke. Utafiti uliofanywa kwa watu 375 huko Hong Kong uligundua kuwa kutumia muda wako wa ziada kufanya kazi za hisani kunasaidia kupunguza hisia za upweke, hasa miongoni mwa wazee.

Nchini Australia na Uholanzi, serikali zinawekeza katika jumuiya za makazi ya kijamii, ambapo wazee na vijana wanahimizwa kujumuika na kushiriki katika shughuli za pamoja, kama vile katika vituo vya jumuiya au maeneo ya umma.

Madaktari nchini Uingereza wanaposhuku wagonjwa wao wanapitia upweke, huwaelekeza shughuli za kijamii ambazo zinaweza kuwasaidia kuwaunganisha watu.

Mwanasaikolojia wa watoto na vijana Dk. Leung Ho Lan, mwandishi wa kitabu "Sense of Belonging," anasema, kujenga jumuiya yenye kushirikiana, ambapo kila mtu ana nafasi, ndilo jambo linalofaa zaidi. Vilevile, kusaidia wengine, pamoja na kukuza huruma, kunaweza kuzuia hisia za upweke."

Ili kuondokana na upweke, kila mtu anapaswa kuzingatia furaha yake na kutosheka, na kutunza urafiki na uhusiano na watu walio karibu naye.

Wanapaswa pia kuzichunguza wenyewe dalili za upweke, kama vile msongo wa mawazo wa muda mrefu au kutotaka kwenda nje na kutotaka kukutana na watu.

Kujitenga ni jambo baya?

A person putting a plant in a pot

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mambo mengi ya kujifurahisha yanaendana vyema na maisha ya kujitenga, kama vile kusoma na kulima bustani

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Reading nchini Uingereza wamegundua kuwa kujitenga mara moja moja kuna athari chanya na hasi katika maisha ya watu.

Utafiti huo ulifuata watu wazima 178 kwa muda wa siku 21, ambao walijaza dodoso na kuweka kumbukumbu ili kupima viwango vyao vya msongo wa mawazo, kuridhika na maisha, hisia za uhuru na upweke.

Matokeo yalionyesha kuwa kadiri watu walivyokaa peke yao kwa muda mrefu, ndivyo walivyokuwa na msongo wa mawazo kidogo na walijisikia huru. Ni dalili za amani ya ndani inayotokana na kujitenga.

Hata hivyo, baadhi ya washiriki waliripoti kwamba siku walizokaa muda mrefu wakiwa peke yao, walihisi kukosa furaha na kutoridhika, na hizo ni dalili za upweke.

Utafiti mwingine unathibitisha kujitenga kunaweza kuwapa watu nafasi ya kudhibiti hisia zao, kujisikia huru na hali ya kujitegemea. Kujitenga ni njia muhimu ya kushughulika na viwango vya juu vya msongo wa mawazo au kushughulika na siku yenye shughuli nyingi.

Kwa maana hii, kujitenga kunaweza kusaidia afya ya akili. Wataalamu wanasema ni muhimu kujenga mazoea au tabia ya mara kwa mara, ya kuweka muda wa kutotazama runinga au kuacha kutumia mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, kujitenga kuna mipaka yake. Utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Reading umegundua kuwa watu huhisi upweke na kutoridhika zaidi siku ambazo hutumia saa nyingi peke yao.

Wataalamu wanasema hakuna muda maalumu wa mtu kujitenga hadi atakapo anza kuhisi upweke. Igawa utafiti unaonyesha wanadamu huanza kuhisi upweke wanapokuwa peke yao kwa zaidi ya 75% ya saa zao za kuwa macho.

Kuhusu shughuli za kufanya ukiwa peke yako, wataalam wanapendekeza ufanye shughuli za kuzuia kusinzia, lakini pia zinazotoa utulivu na kusaidia kupunguza msongo wa mawazo.

Mambo mengi ya kujifurahisha yanaendana vyema na maisha ya kujitenga, kama vile kusoma, kulima bustani, matembezi, kusikiliza muziki, kupika, na kufanya aina mbalimbali za kazi za mikono.