Fainali Europa: Man United na Spurs katika vita ya mwisho ya ukombozi

s

Katika msimu ambao umekuwa wa maumivu makali kwa mashabiki wa Manchester United na Tottenham Hotspur, fainali ya Europa League mjini Bilbao leo usiku imebeba maana kubwa kuliko tu taji la Ulaya. Ni mechi ya ukombozi. Vikosi hivi viwili vya Kiengereza vimekuwa vikipambana si tu dhidi ya wapinzani wao, bali pia dhidi ya historia, matarajio, na uhalisia mchungu wa msimu wa 2024-25.

United na Spurs wanaingia fainali hii wakiwa kwenye nafasi ya 16 na 17 mtawalia katika msimamo wa Ligi kuu England, matokeo mabaya kabisa kwa klabu hizi tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo. Kwa pamoja, zimekusanya jumla ya vichapo 39 kwenye ligi na kushinda mechi 21 pekee.

Kwa Man United, tayari ni hakika kuwa hii ndiyo itakuwa nafasi yao mbaya zaidi ya kumaliza msimu wa ligi katika historia ya EPL. Kwa Spurs, lazima wapande angalau nafasi tatu ili kuepuka kuwa na msimu mbaya zaidi wa ligi katika historia yao.

Katika mazingira haya ya majonzi, kocha wa Spurs Ange Postecoglou na mwenzake wa United Ruben Amorin wanakabiliwa na shinikizo kubwa. Kauli mbiu ya "kutwaa kombe" haijawahi kuwa na uzito kama sasa.

Ikiwa mmoja wao hatafanikiwa kutwaa taji leo, kuna uwezekano mkubwa wa kufukuzwa kazi kabla ya msimu mpya kuanza. Ni fainali inayoweza kuamua mustakabali wao kama makocha na huenda ikawa kipimo cha mwisho kwa imani ya uongozi wa klabu na mashabiki wao.

"Huwa nashinda kombe katika msimu wangu wa pili"

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ange Postecoglou

Ange Postecoglou aliitupia dunia kauli hii kwa kiburi mwezi Septemba mwaka jana, baada ya kupoteza dhidi ya Arsenal nyumbani kwa bao 1-0. Ilionekana kuwa porojo ya kujifariji wakati huo lakini miezi minane baadaye, Spurs wako fainali ya Europa Ligi huku kocha wao akiwa na nafasi ya kuitimiza ahadi hiyo.

Ni fainali inayoweza kuhitimisha ukame wa miaka 17 wa Spurs bila kuwaa taji lolote tangu walipotwaa kombe la ligi (Carling Cup) mwaka 2008. Lakini fainali hii ni njia ya kuwaingiza moja kwa moja katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Hata hivyo, Spurs msimu huu imekuwa na msimu mbovu ukiacha kufika fainali hii. Wamepoteza michezo 25 katika mashindano yote, na kufikia rekodi yao ya msimu wa 1991-92. Katika ligi kuu pekee, wamefungwa mara 21, ikiwa ni rekodi ya kihistoria. Lakini kama watashinda leo, huenda makosa na matokeo hayo mabovu yote yatasahaulika. Ushindi huu unaweza kumpa Postecoglou hadhi ya kuwa "mkombozi" lakini pia utaleta mtihani mgumu kwa mwenyekiti Daniel Levy: je, aendelee naye licha ya msimu wa kusuasua?

Bruno Fernandes tishio dhidi ya viungo na beki za Spurs

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bruno

Ikiwa kuna mchezaji ambaye Spurs wanapaswa kumlinda kwa uangalifu wa hali ya juu, basi ni Bruno Fernandes. Nahodha huyo wa United ameweka historia katika michuano Europa League:

  • Ndiye mchezaji aliyetengeneza mabao mengi zaidi (19)
  • Ushiriki wa moja kwa moja katika mabao 46
  • Ametengeneza nafasi 32 katika hatua ya mtoano

Fernandes sio tu injini ya timu, bali ni mchezaji wa mechi kubwa. Akiwa na uwezo wa kusambaratisha safu yoyote ya ulinzi kwa pasi au shuti moja, uwepo wake leo unaweza kuwa tofauti kati ya huzuni na furaha kwa mashabiki wa United. Ikiwa atakuwa katika kiwango chake cha kawaida, basi Spurs wana kazi ya ziada ya kumdhibiti.

Chini ya Postecoglou, Spurs wamekuwa na matatizo mengi, lakini kutengeneza nafasi. Katika ligi luu msimu huu, licha ya kufanya vibaya ni timu nne tu zilizofunga mabao mengi zaidi, yale yasiyo ya penalti (61).

Hata hivyo, wanaingia fainali Bilbao wakikabiliwa na tatizo la kipekee: wachezaji wao watatu bora, viungo washambuliaji wote wameumia, James Maddison, Dejan Kulusevski, na Lucas Bergvall.

Pengine Yves Bissouma, Rodrigo Bentancur na Pape Sarr watakuwa na kazi kubwa kulinda safu ya ulinzi na kusaidia kupunguza madhara ya Bruno Fernandes kwenye lango lao.

Yeyote atakayeshinda Europa Ligi ataandika historia

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kombe la Europa linalowaniwa

Yeyote atakayeshinda fainali ya Europa ligi leo ataweka rekodi mpya kwa kuwa timu iliyo katika nafasi ya chini kabisa katika msimamo wa ligi yao ya nyumbani kuweza kushinda taji kubwa la Ulaya.

Hakuna hata timu moja kati ya washindi 177 waliopita waliotwaa mataji ya Ulaya ya Ligi ya Mabingwa, Kombe la UEFA/Inter-Cities Fairs Cup/Europa League, au Conference League aliyewahi kumaliza chini ya nafasi ya 14 katika ligi yao ya nyumbani msimu huo. Rekodi inayoshikiliwa sasa na West Ham United waliposhinda Conference League ya 2022-23 na kumaliza wa 14 katika Ligi Kuu.

Katika mashindano haya (pamoja na wakati ule ilipokuwa Kombe la UEFA), ni Inter Milan pekee ambao wanashikilia rekodi ya kumaliza ligi katika nafasi ya chini kabisa huku wakishinda taji. Walimaliza wakiwa nafasi ya 13 katika Serie A katika msimu wa 1993-94 lakini pia waliitandika klabu ya Austria SV Casino Salzburg 2-0 katika mechi mbili za fainali ya Kombe la UEFA na kutwaa taji hilo.

Man United na Spurs zilizo nafasi ya 16 na 17 sasa zitaandika historia mpya kwa timu iliyofanya vibaya zaidi kwenye ligi lakini ikatwaa kombe kubwa la Ulaya.

Lakini pia timu itakayoshinda itamaliza msimu na taji la Uropa na kupata nafasi katika Ligi ya Mabingwa kwa msimu ujao wa 2025-26.

Katika msimu huu timu hizo zimekutana mara tatu na mara zote Spurs imeshinda.

Mara ya sita Vilabu vya England kukutana Ulaya

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mshambuliaji wa Ufaransa wa Chelsea, Olivier Giroud, akishangilia kombe la Europa ligi baada ya kuwafunga Arsenal katika Uwanja wa Olimpiki wa Baku huko Baku, Azerbaijan, mnamo Mei 29, 2019

Mechi ya leo inakuwa mara ya sita kwa vilabu vya England kukutana katika fainali ya michuano ya Ulaya. Hii si tu heshima kwa soka la Kiingereza bali pia ni kipimo cha uthabiti wa vilabu hivi licha ya kuwa na misimu ya hovyo ndani ya nchi.

Mechi zingine zilizokutanisha timu za Uingereza kwenye fainali ya Ulaya kihistoria kama Ligi ya mabingwa Ulaya, (UCL), Europa ligi (UEL) ama zamani Kombe la UEFA (UEFA Cup) ni:

  • Chelsea 1-0 Man City (UCL, 2021)
  • Spurs 0-2 Liverpool (UCL, 2019)
  • Chelsea 4-1 Arsenal (UEL, 2019)
  • Man United 1-1 Chelsea (UCL 2008, Man U alishinda 6-5 kwa penati)
  • Spurs 3-2 Wolves (UEFA Cup, 1972 – fainali ya mikondo miwili)

Tofauti na fainali zilizopita, mechi ya Spurs vs United inakutanisha vilabu vilivyokuwa dhaifu msimu mzima lakini vinapigania kutengeneza heshima Ulaya.

Manchester United na Spurs wamekuwa na kampeni za ligi mbaya kihistoria. Kwa msimu wa 2024-25 tayari umethibitisha Man Utd atamaliza na alama za chini kabisa katika msimu wa ligi tangu mwaka 1973-74, na endapo watashindwa kuifunga Aston Villa katika mechi ya mwisho ya msimu, itakuwa rekodi yao mbaya zaidi tangu msimu wa 1930-31 (walipopata alama 29).

Spurs wao wana alama 38 tu katika mechi 37 za ligi msimu wa 2024-25, na iwapo watapteza mechi yao ya mwisho ya msimu dhidi ya Brighton, itakuwa kampeni yao ya pili mbaya zaidi ya ligi katika historia baada ya ile ya 1914-15 (alama 36). Sasa wamepoteza mechi 25 katika mashindano yote msimu huu, idadi yao kubwa zaidi ya vipigo katika msimu mmoja katika historia yao ikilingana na ile ya msimu wa 1991-92 ilipopogea vipigo 25).

Kuelekea siku ya mwisho ya kampeni ya Ligi kuu mwishoni mwa wiki hii, United na Spurs wako mkiani katika msimamo, United ya 16 na Spurs ya 17, nafasi za chini kabisa baada ya zile tatu zilizoshuka daraja.

Sasa fainali ya leo ni tofauti kidogo: si vita ya kifahari, bali ni sawa na pambano la mwisho la vilabu vilivyokata tamaa. Kwa Spurs, ni nafasi ya kuandika upya historia ya Ulaya baada miaka 41. Kwa United, ni tumaini la pekee la kubeba taji la kwanza chini ya Ruben Amorim.

Kwa hiyo katika mji wa kihistoria wa Bilbao huko Hispania, leo usiku si tu hatima ya kombe inayotazamwa, bali historia mpya ya klabu moja wapo itazaliwa. Kati ya Tottenham na Manchester United, ni nani ataibuka shujaa wa ukombozi?