China na Taiwan: Je, mazoezi ya China karibu na Taiwan yanatoa ujumbe gani?

Chanzo cha picha, EPA
Ziara ya spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi imezua mvutano mpya kati ya Taiwan inayojitawala yenyewe na China, ambayo inadai kisiwa hicho ni sehemu ya ardhi yake. Waandishi wa BBC wanapima umuhimu wa jibu la China baada ya ziara hiyo ambayo ni mazoezi yake ya kijeshi ya moja kwa moja kuzunguka kisiwa hicho.
Kawaida mpya
Stephen McDonell, Beijing
Washikadau wenye msimamo mkali katika ngazi za juu za Chama cha Kikomunisti cha China pengine wamefurahishwa sana na namna ambavyo ziara ya Nancy Pelosi imewaacha.
Pelosi aliwapa dirisha na wakalitumia.
Msururu wa hatua kali zaidi za kijeshi karibu na Taiwan sasa zimeingizwa kwenye ulimwengu wa "kukubalika".
Hatua hizi ikiwa ni pamoja na kurusha makombora katika kisiwa hicho - zimekuwa "zinazokubalika" sio kwa sababu jumuiya ya kimataifa inazikubali lakini kwa sababu zimefanyika na Beijing imejitoa.
Kila wakati Jeshi la Ukombozi wa Watu (PLA) linaporusha ndege za kivita karibu au kwa wingi zaidi katika Mlango wa Bahari wa Taiwan, inakuwa katika kiwango kipya.
Zaidi ya hayo, wazo lenyewe kwamba China inaweza siku moja kushambulia Taiwan ili kuteka eneo hilo kwa nguvu sasa linachukuliwa kuwa jambo linalowezekana kwa Wachina wengi zaidi.
Tena, hii inaonekana kama ushindi kwa wale wanaotaka ifanyike.
Mikakati mingine ya amani zaidi ya kufikia kile Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi alielezea kama "kurejea kwa Taiwan katika nchi mama" haijadiliwi kwa sasa au bila shaka haijajadiliwa kwa undani wowote.
Manufaa ya zoezi hili kuu na la moja kwa moja la jeshi la PLA pia imekuwa kuzidisha imani duniani kote kwamba kukua kwa kijeshi la China hakuzuiliki,- hii inaweza kuwatisha majirani wa Kusini Mashariki mwa Asia ambao wana madai pinzani kwa Bahari ya China Kusini.
Mazoezi haya makubwa ya kijeshi yamechukua mipango fulani. Ni vigumu kufikiria kwamba majenerali walitunga yote hayo kwa ghafla, ilipofichuliwa kwamba Pelosi alikuwa akipanga kutembelea Taiwan.
Kinachoonekana zaidi ni kwamba walikuwa na mipango tayari na waliitoa nje ya droo kwa sababu fursa ilijitokeza yenyewe.
Kama raia mmoja huko Beijing alivyosema alipohojiwa mtaani wiki iliyopita, "Asante comrade Pelosi"!

Chanzo cha picha, Reuters
Itakuwa hatari kama serikali ya China itashikilia sana na maneno yake ya kivita na kuanza kujiaminisha kuwa kuishikilia na kuidhibiti Taiwan kunaweza kuwa rahisi badala ya tukio gumu, la umwagaji damu na janga.
Baadhi ya wachambuzi hata wanafikiri kwamba michezo hii ya kivita imesaidia jeshi la Taiwan na Marekani katika kuandaa mikakati ya ulinzi ili kuzuia mashambulizi yoyote kutoka bara.
Lakini mazoezi hayo hayakutosha kwa serikali ya Rais Xi Jinping. Siku ya Ijumaa usiku wizara ya mambo ya nje ilitangaza kuwa China inasitisha ushirikiano na Marekani kuhusu uhalifu wa kuvuka mipaka, ikiwa ni pamoja na dawa za kulevya na usalama wa baharini, na kwamba mazungumzo yote ya ngazi ya juu ya kijeshi kati ya Marekani na China yangesitishwa.
Vyombo vya habari vya Marekani pia vimeripoti kwamba simu za Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin, na Jenerali Mark Milley, mwenyekiti wa wakuu wa pamoja wa wafanyakazi, hazikujibiwa kutoka upande wa China.
Muhimu zaidi, Beijing imesitisha ushirikiano kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na Washington. Hivyo watoa hewa chafu ya kaboni wakubwa zaidi duniani hawazungumzi.
Mvutano umeongezeka kufuatia ziara ya Pelosi, lakini serikali ya Xi inaonekana kupenda hivyo angalau kwa sasa.
Vita vya maneno
Rupert Wingfield-Hayes, Taiwan Kwa siku chache zilizopita, umakini mkubwa umekuwa kwenye fataki za kijeshi zinazoendelea karibu na Taiwan. Lakini muhimu vile vile ni maneno kutoka Beijing ambayo yameambatana na mazoezi.
Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi ametaja kundi dogo la wanasiasa wa Taiwan ambao amewaita kuwa "vikosi vya kujitenga vya Taiwan".
Wa juu katika orodha hii ni Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen. Ametajwa kwa nafasi maalum. Waziri Wang alimwita "mzao asiyestahili wa taifa la China" - kwa maneno mengine, msaliti.
Kusudi ni kujaribu kutenganisha umati wa watu wa Taiwan, ambao China inasema sio adui, kutoka kwa "kikundi" kidogo ambacho kinadai kinajaribu kuiondoa Taiwan kutoka kwa nchi mama.
Shida ya Beijing ni toleo hili la Taiwan halipingani kabisa na ukweli. Kura za maoni za hivi majuzi zinaonyesha idadi kubwa ya WaTaiwani wanapinga aina yoyote ya kuungana na China, na wengi wanaokua wanajiona "WaTaiwani" na sio "Wachina".
Kulingana na Wang Yi, hii ni kwa sababu serikali ya Tsai Ing-wen imekuwa "ikishawishi kuondoa utamaduni wa wachina wengi wa Sinicisation" na kujaribu kuunda "China mbili" au "China moja, Taiwan moja".

Chanzo cha picha, EPA
Ndiyo maana tumemsikia balozi wa China nchini Ufaransa akisema kwamba baada ya Taiwan "kuunganishwa" na China, watu wa Taiwan "watahitaji kuelimishwa upya". Kwa mujibu wake, "wamebadilishwa kiakili" kwa kuamini kuwa wao sio Wachina.
Tena, hii inapingana kabisa na ukweli. Taiwan ni jamii iliyo wazi ambapo watu wako huru kusoma wanachotaka, kufikiria wanachotaka, na kupiga kura kwa wale wanaopenda.
Swali sasa ni: haya yote yatakuwa na athari gani?
Madhumuni ya Beijing ni kuwatia hofu WaTaiwan katika kupiga kura dhidi ya chama cha Rais Tsai katika uchaguzi ujao mwaka wa 2024. Wangependa kuona KMT (Kuomintang) yenye urafiki zaidi na China ikirejea madarakani.
China pia inatoa vitisho vya moja kwa moja kwa viongozi wa biashara wa Taiwan, ambao wengi wao wana uwekezaji mkubwa katika bara la China. Wanaambiwa wanahitaji "kuchagua upande wa sahihi".
Beijing imejaribu aina hizi za mbinu hapo awali, na hazijafanikiwa sana. Biashara nyingi za Taiwan zitaumizwa na vikwazo vya Beijing, haswa wakulima wake wa matunda. Sekta ya utalii tayari inaumizwa na vikwazo vya China kwa watalii wa bara wanaokwenda Taiwan.
Lakini ikiwa ushahidi wa siku chache zilizopita ni jambo la kupita, mitazamo ya Taiwan kuelekea Beijing inaonekana kuwa migumu zaidi.