Israel na Hezbollah: Athari ya uvamizi wa kijeshi wa Israel kwa pande zote mbili

Chanzo cha picha, EPA
Vyombo vya habari vya Israel viliwanukuu maafisa wa jeshi la Israel wakisema kuwa hatua ya msingi ya kuingia eneo la kusini (kuelekea Lebanon) ni suala la muda tu.
Walla alisema kuwa ingawa uamuzi bado haujafanywa katika ngazi ya kisiasa, jeshi liko tayari kwa uvamizi wa ardhini.
Wiki iliyopita, Mkuu wa Majeshi wa Israel alitoa wito kwa wanajeshi wake kujiandaa "kuingia " huko Lebanon, wakati jeshi la Israel lilipotangaza kuwa limeita brigedi mbili za akiba kwa "misheni ya operesheni" kaskazini.
Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Galant hapo awali aliahidi kuwarejesha wakazi wa kaskazini mwa Israel katika makazi yao, na kusisitiza kuwa kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya Hezbollah kumeingia katika hatua mpya huku rasilimali zaidi zikielekezwa upande wa kaskazini.
Jumatatu iliyopita, ongezeko hilo lilifikia hatua muhimu kutokana na kupanuka kwa wigo na ukubwa wa mashambulizi ya Israel nchini Lebanon. Mtazamaji yeyote wa tukio atajiuliza ikiwa mambo yatasababisha kuongezeka zaidi kwa operesheni ya ardhini ya Israel ndani ya Lebanon.
Je, uvamizi wa Lebanon ungekuwaje kama ungetokea?
Katika vita vya awali nchini Lebanon, Israel imefuata mbinu mbalimbali katika operesheni zake za ardhini, kulingana na mabadiliko ya mazingira ya vita.
Vita vya 1982 - Uvamizi wa Ardhini:
Katika vita vya 1982, maelfu ya wanajeshi, wakiandamana na mamia ya vifaru na magari ya kivita, walivuka mpaka kati ya Lebanon na Israel.
Uvamizi huo ulikuwa mkubwa, na uliendana na mashambulizi makali ya anga, majini na mizinga.
Vikosi vya Israel vilipenya katika nyanja nyingi na viliweza, ndani ya wiki moja, kufika kwenye viunga vya mji mkuu, Beirut, na kuuwekea mzingiro.
Kisha uvamizi huo ulilenga pande kuu tatu, mbili zikianzia eneo linalojulikana kama Galilaya kuelekea Bonde la Bekaa mashariki mwa Lebanoni na maeneo ya milimani ya kati, na upande wa tatu ulikuwa kando ya barabara ya pwani kutoka kusini hadi Beirut.
Uvamizi huo pia ulijumuisha kuingia kwa jeshi la majini la askari wa miguu na magari ya kivita kaskazini mwa mji wa Sidoni.
Uvamizi wa ardhini mwaka 2006 ulikuwa mdogo na kwa kasi ndogo ikilinganishwa na 1982, na ulizuiliwa kwenye miji ya karibu ya Lebanon na mazingira yake ndani ya ukanda wa mpaka, na kwa kina kisichozidi kilomita chache ndani ya Lebanon.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Israel Yoav Stern alikataa, wakati wa mahojiano yake na BBC, kwamba hali ya uvamizi ujao wa ardhini itakuwa sawa na kile kilichotokea mwaka wa 1982, na alisema kuwa "utakuwa uvamizi wa tahadhari na wa mahesabu, ikiwa ni pamoja na uvamizi wa miji ya kusini mwa Lebanon moja baada ya nyingine, badala ya kuanzisha uvamizi wa haraka na wa kina.
Itakuwa sawa na kile kilichotokea mwaka wa 2006, lakini ndani zaidi ya eneo la Lebanon, kufikia Mto Litani.
Stern alihusisha matarajio yake na ukweli kwamba Hezbollah imekuwa katika miji ya kusini mwa Lebanon kwa muda mrefu, ambayo inazuia uwezekano wa kuikalia miji hii.
Brigedia Jenerali Hisham Jaber, mkuu wa Kituo cha Mashariki ya Kati cha Mafunzo na Utafiti huko Beirut, alikataa wakati wa mahojiano yake na BBC kwamba Israeli itavamia kusini mwa Lebanoni na kusalia huko kwa muda mrefu, kwani Israeli ilipata matokeo ya uvamizi wa ardhini huko. 2006 na kabla. Kwa hivyo, Brigedia Jenerali Jaber anaamini kuwa aina ya uvamizi huo itakuwa mbali na kile kilichotokea mnamo 1982 au 2006.
Brigedia Jenerali Jaber anatarajia kwamba operesheni za ardhini za Israel nchini Lebanon zitahusu tu uvamizi wa kuvuka mpaka katika wigo finyu sana unaojumuisha maeneo machache, na kwamba kila uvamizi ambao Israel inaweza kufanya hautazidi siku moja.
Brigedia Jenerali Jaber anaamini kuwa Israel itaachana na uvamizi wa ardhini kwa kuendelea kuzidisha mashambulizi yake ya anga, kutekeleza mauaji na operesheni za usalama mtandaoni.
Uvamizi wa ardhini utakuwa wapi?
Katibu Mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah, katika hotuba yake Alhamisi iliyopita kufuatia shambulio la vifaa vya mawasiliano huko Lebanon, alijibu pendekezo la afisa wa kijeshi wa Israel kuhusu uvamizi wa Lebanon ili kuweka ukanda wa usalama ndani ya ardhi yake, akisema kuwa kile Israel inakiona kuwa tishio kwa kuanzisha ukanda wa usalama, Hezbollah inaona kama "fursa ya kihistoria ambayo itakuwa na athari kubwa kwenye vita."
Katika hotuba yake, Nasrallah alirejea ukanda wa usalama ambao Israel ilianzisha mwaka 1978 kusini mwa Lebanon, akimaanisha eneo la mpaka kati ya Lebanon na Israel.
Brigedia Jenerali Jaber, ambaye awali aliondoa hali ya uvamizi wa ardhini, anatazamia kuwa operesheni za ardhini za Israel, ikiwa zitatokea, zitahusu "maeneo machache sana katika miji ya mpakani mwa Lebanon."
Stern, kwa upande mwingine, anatarajia wigo wa operesheni ya ardhini inayoweza kujumuisha kusini mwa Lebanon, ambayo ni eneo kati ya mpaka wa Lebanon na Israel na Mto Litani, lakini hakupuuza kwamba mazingatio ya kimbinu yanaweza kuilazimisha Israel kupenya.
Malengo ya uvamizi yatakuwa yapi?
Malengo yaliyotangazwa ya vita vya 1982 na operesheni zake za ardhini ilikuwa ni kuondoa miji ya kaskazini mwa Israel kutoka kwenye safu madhubuti ya maroketi na makombora yaliyorushwa na wapiganaji wa Palestina kusini mwa Lebanon, kwa kuwasukuma kilomita 40 kutoka mpaka wa Lebanon na Israel, pamoja na kuharibu miundombinu ya Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina, ikiwa ni pamoja na makao yake makuu huko Beirut, na kusukuma vikosi vya Syria kutoka Lebanon, kwa mujibu wa Israel.
Shambulio la Israel mwaka 1982 halikuishia kusini mwa Lebanon pekee, bali lilijumuisha maeneo mapana ya Bekaa, Milima ya Chouf na Beirut.
Stern anaamini kwamba Israel kimsingi italenga, kupitia uvamizi wowote unaowezekana kusini mwa Lebanon, kuwasukuma wapiganaji wa Hezbollah kaskazini mwa Mto Litani, kwa sababu kuu mbili: "kuzuia urushaji wa makombora ya masafa mafupi kuelekea miji ya Israel, na kuzuia kutokea tena. shambulio kama lile la Oktoba 7 kaskazini mwa Israel.
Katika hotuba yake, Hassan Nasrallah alidokeza kuwa Israel inafikiria kuanzisha ukanda wa usalama ndani ya Lebanon, kwa lengo la kugeuza mwelekeo wa Hezbollah na kuiburuza ili kuelekeza operesheni zake ndani ya ukanda huu mbali na kaskazini mwa Israel, lakini alisisitiza kwamba "haitazuia Hezbollah" kutekeleza operesheni dhidi ya maeneo ya kijeshi na miji ndani ya Israel."
Je, uvamizi utadumu kwa muda gani?
Awamu ya kwanza ya uvamizi wa 1982 ilidumu takribani miezi 3, na ilimalizika kwa kuondoka kwa wapiganaji wa PLO kutoka mji mkuu wa Lebanon Beirut mwishoni mwa Agosti mwaka huo huo. Kuhusu vita vya 2006, shughuli za mapigano ya ardhini zilidumu kwa siku 27.
Stern anaamini kuwa Israel imebadili mtazamo wake kwa operesheni za kijeshi.
Hapo awali, ilitegemea zaidi vita vifupi, lakini vita vinavyofuata vinaweza kuwa vya muda mrefu.