Baba ambaye alitoa watoto wake watatu kwa serikali ya Korea Kaskazini

m

Chanzo cha picha, YONGHI-YANG

Mtengeneza filamu wa Kikorea Yonghi Yang alikulia Japani miaka ya 1960, kama sehemu ya jamii kubwa ya wahamiaji kutoka nchi yake ya kuzaliwa ambayo ilikuwa na makazi katika jiji la Osaka.

Wakiwa wamechoshwa na kuvumilia chuki dhidi ya Wakorea nchini Japan na wakichochewa na ahadi ya serikali ya Korea Kaskazini ya kuunda paradiso ya uongozi wa kisoshalisti, wazazi wake walifanya uamuzi wa kuwatuma wana wao watatu kwenda Korea Kaskazini mapema miaka ya 1970 kama zawadi ya siku ya kuzaliwa kwa kiongozi Kim Il-Sung.

Wakati ndugu zake walienda kuishi katika mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang, Yonghi alikaa na wazazi wake na ametumia muda mwingi wa maisha yake kujaribu kuelewa uamuzi huo na matokeo yake. Na amejitolea kutengeneza filamu kuhusu maisha yake, ya hivi punde zaidi ikiitwa Soup and Ideology.

Yang alikiambia kipindi cha Outlook cha BBC hadithi hiyo.

Siku ambayo ndugu zangu wawili walitumwa Korea Kaskazini kama zawadi kwa mapinduzi, mwanzoni nilifikiri ilikuwa safari ya familia ambapo sote tungeenda kujiburudisha.

Tukavaa mavazi ya kitamaduni. Tulikuwa tunaishi Osaka na siku hiyo wazazi wetu walituambia kwamba tulikuwa tukienda ufukweni.

Tulipofika bandarini, tuligundua kuwa kulikuwa na watu wengi zaidi.

Kulikuwa na bendi iliyopiga nyimbo za kutoka nchini mwetu, lakini sikuweza kuona chochote kwa sababu watu wengi waliokuwa pale walikuwa warefu kuniliko.

Nakumbuka kwamba rafiki mmoja wa kaka yangu alinishika na kuniweka begani kwake, ili niweze kuona.

Maelfu ya vipande vya karatasi vya rangi vilianguka kutoka angani. Ilikuwa mwaka 1971 na nilikuwa na umri wa miaka 6.

Siku hiyo, ndugu zangu wawili wangetumwa Korea Kaskazini.

Lakini sikujua wakati huo, nilianza kusikia wakiwaambia kwamba wanapaswa kujivunia kurudi walikozaliwa na kwamba walikuwa watu wazuri.

Ndipo nikagundua kuwa walikuwa wakienda safari. Kitu ambacho sikuweza kufikiria siku hiyo ni kwamba sitowaona kwa muda mrefu.

YONGHI-YANG

Chanzo cha picha, YONGHI-YANG

Walikuwa wadogo sana. Mmoja alikuwa na umri wa miaka 14 na mwingine 16.

Nakumbuka kulikuwa karamu ya kuaga ndugu zangu, marafiki zao, majirani. Kila mtu aliwatakia mafanikio na kazi njema huko Korea Kaskazini.

Nilikuwa na huzuni sana, lakini sikuweza kusema chochote kwa sababu watu wazima walihusika katika kuwaaga.

Wazazi wangu walionekana kufurahishwa na wazo kwamba watoto wao wangesaidia kujenga paradiso ya kisoshalisti.

Mwaka mmoja baadaye, kaka yangu mkubwa, ambaye alikuwa na umri wa miaka 18, alijiunga na wale wengine wawili huko Pyongyang kama zawadi kwa kiongozi wa mapinduzi, Kim Il-Sung.

Hii ilitokea kwa sababu katika chuo kikuu nilichosoma na ambacho kilikuwa kinaunga mkono Korea Kaskazini, mradi ulitokea wa kuwapa vijana zawadi kwa mapinduzi ambapo 200 walichaguliwa.

Karibu nusu walisema hawataki kwenda Korea Kaskazini.

Kutokana na hali hiyo, shinikizo kwa ndugu zangu kurejea katika nchi yao ya asili ilianza kuongezeka

Lakini alichosema yeye na ndugu zangu wengine ni kwamba hata wazazi wetu hawakutoka huko.

Mizizi yao ilikuwa kusini mwa nchi na walikuwa wamehamia Japani pamoja na familia yao. Haya yote yalitokea kabla ya mgawanyiko wa Korea mbili, katika miaka ya 1950.

Korea moja

Wakati huo, Korea ilikuwa sehemu ya ufalme wa Japani na familia nyingi za Wakorea zilisafiri hadi Japan na wazo la kutafuta maisha bora. Kati ya hizo ilikuwa ni familia yangu.

Kama familia zingine nyingi zilizohama, tulilazimika kuishi katika maeneo ya Kikorea, kwenda shule za Kikorea, kila kitu ili kuendelea kuishi na utamaduni wa nchi yetu.

Wazazi wetu walifunga ndoa huko Japan na kuhamia jiji la Osaka, ambako kulikuwa na jamii kubwa ya watu wa nchi hiyo.

Lakini hapakuwa mahali rahisi kwetu.

Kulikuwa na ubaguzi mwingi, pia, hatukuruhusiwa kuwa raia wa Japan kwa hiyo wengi wetu tuliishi katika umaskini bila kupata kazi nzuri.

Lakini, baada ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, Korea iligawanywa katika sehemu mbili: Kaskazini, ikiungwa mkono na Umoja wa Kisovieti, na Kusini, ikiungwa mkono na Marekani.

Sisi Wakorea tulioishi Japani tulipaswa kuchagua kati ya kaskazini na kusini.

YANG

Chanzo cha picha, YANG

Na sasa inaonekana kuwa jambo la kushangaza, lakini kwa miaka michache, haswa baada ya kugawanyika, Korea Kaskazini ilikuwa ya kuvutia zaidi.

Ghafla ikawa paradiso yenye matumaini.

Kwa hiyo wazazi wangu, wakishawishiwa na wazo hilo, waliunga mkono mradi wa Korea Kaskazini na hawakutoa uaminifu wao tu bali pia watoto wao.

Kwa hiyo nilichosikia nilipokuwa nawaaga ndugu zangu wawili ni kwamba walitaka kurudi Korea Kaskazini ili kuwa na maisha bora.

Hata hivyo, waliamua kutonituma kwa sababu nilikuwa mdogo. Kutoka hapo walianza kuitangaza nchi kupitia shirika la kitamaduni walilokuwa nalo.

Nyufa

Baadaye tulitambua kwamba paradiso ambayo wazazi wangu waliamini sana ilikuwa msiba. Na kwamba uamuzi wa kuwapeleka ndugu zangu Korea Kaskazini ulikuwa wa makosa.

Walitutumia barua na picha mara kwa mara. Walituambia kwamba walikuwa na furaha, walishukuru Korea Kaskazini na kutuhakikishia kwamba kila kitu kinaendelea vizuri, na kwamba walikuwa wakisoma kwa bidii sana.

Lakini kwenye picha tuliona kitu kingine. Mama yangu aligundua kuwa mdogo wangu alikuwa amekonda sana na ni kama aliathiriwa na njaa, kiasi kwamba alianza kulia na kuamua kuvunja picha.

Mama yangu aliwatumia vifurushi vilivyojaa vifaa katika miaka ya 1980 na hasa katika miaka ya 1990, wakati nchi ilikumbwa na njaa.

Lakini hakuwatumia pesa, kwa sababu hata kama walikuwa na pesa, hazikuwa na matumizi mengi: hakukuwa na kitu cha kununua. Kwa hiyo masanduku aliyowapelekea yalikuwa yamejaa mafuta, sukari na nguo.

Nakumbuka nilipokuwa shuleni nikiwa kijana, nilianza kuwaambia wazazi wangu kwamba sikuskia vizuri kuhusu ndugu zangu kuwa Korea Kaskazini.

YONGHI-YANG

Chanzo cha picha, YONGHI-YANG

Niliwapenda sana wazazi wangu, lakini nilianza kuhisi kwamba sitaki kufuata itikadi zao. Sikutaka hilo.

Yaani nilianza kukataa wazo la kuwa nifanye mambo kwa ajili ya nchi yangu au taasisi zake. Sikutaka kuwa na uhusiano na serikali ya Korea Kaskazini.

Na ulikuwa uamuzi ambao nilithibitisha wakati wa safari niliyofanya na shule yangu kwenda Pyongyang.

Wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 17 na sikuwa nimewaona ndugu zangu kwa miaka 11. Na tuliweza kuonana, lakini kwa muda mfupi tu, sikuweza kuwa nao katika nyumba zao.

Badala yake, nilitumia saa nyingi kutembelea makumbusho na mahali tulipofundishwa kuhusu historia ya mapinduzi.

Tuliweza kufanya mikutano ya dakika 20 pekee na hilo lilikuwa jambo ambalo lilinishangaza sana kwa sababu ya muda mchache waliotupatia.

Pia nakumbuka nililia sana nilipowaona mara ya kwanza.

Jambo lingine lililonibana ni kwamba hawakutaka kuzungumzia masuala ya kisiasa.

Kila tulipozungumza, tulifanya hivyo tukifikiri kwamba tunarekodiwa, hasa tukiwa kwenye lango la hoteli niyokuwa ninaishi.

Wakati pekee tuliweza kuzungumza kwa utulivu zaidi ni tulipokuwa nje kwa matembezi. Lakini hata hivyo kaka yangu mkubwa alipendelea kutozungumza juu ya masuala magumu.

Nilichoona kwenye safari hiyo ni tofauti kubwa kati ya Pyongyang na miji mingine iliyozunguka jiji kuu.

m

Chanzo cha picha, Getty Images

Havikuwa kama vitongoji vya Japan, vilikuwa maskini sana.

Nilichojifunza baadaye ni kwamba kulikuwa na watu ambao walichaguliwa kuishi Pyongyang, pamoja na starehe za jiji, na wengine walilazimika kuishi vijijini.

Muda si muda wazazi wangu waliweza pia kuwatembelea watoto wao.

Ilikuwa wakati wa ziara hizo ambapo mama yangu alianza kuelewa jinsi kaka zangu walikuwa wameishi miaka hiyo yote.

Na kadiri alivyozidi kuelewa uhalisia wa Korea Kaskazini, ndivyo masanduku makubwa alivyoyatuma kutoka Japan.

Nilisikia wazazi wangu wakilia pamoja mara nyingi, hasa walipofikiri walikuwa peke yao.

Lakini walipokuwa mbele ya watu wengine, walisema tu kwamba watoto wao walikuwa na furaha katika nchi yao, huko Korea Kaskazini, na kwamba walikuwa wanajivunia watoto wao.

Sasa niliweza kuelewa kwamba hiyo ilikuwa njia bora zaidi ya kuwasaidia ndugu zangu. Walilenga kuwasaidia ili waweze kuishi nchini Korea Kaskazini.

Baada ya safari hiyo na kutafakari kwa miaka kadhaa, nilielewa kwamba kilichonifanya nitengeneze filamu zangu kuhusu suala hili ni kujibu swali: je, baba yangu alihisi hatia kwa kuwapeleka Korea Kaskazini?

m

Chanzo cha picha, Getty Images

Ndugu

Ili kujibu swali hilo, ilinibidi nianze kwa kuona jinsi ndugu zangu walivyohisi baada ya kutumwa huko. Kwa sababu ilionekana kuwa ni ukatili kumuuliza baba swali moja kwa moja.

Wakati huo ndipo nilipochukua kamera na kusafiri hadi Pyongyang.

Lakini jibu la kweli lilikuwa tayari limetolewa kwangu kabla ya kurekodi filamu Dear Pyongyang, ambapo ninasimulia hadithi hii ya wazazi na ndugu zangu.

Kwa muda mfupi tulioweza kuzungumza nilipowatembelea wakati huo nikiwa kijana, walikuwa wamesisitiza sana kwamba nitumie faida ambazo Japan ilinipa.

Baada ya muda nilielewa: Walichoniambia ni kufurahia maisha na kufanya hivyo kwa ajili ya yale ambayo hawakuweza kuwa nayo.

Shida ni kwamba sijaweza kuwaona tena. Tangu tulipotoa filamu hiyo, ambapo tulijadili masuala haya yote, Korea Kaskazini imeipiga marufuku.

Walidai kwamba niombe msamaha hadharani, na kwa kuwa sikufanya hivyo, siruhusiwi kuingia nchi hiyo.

Tangu 2004, nilipoiweka hadharani filamu hiyo, sijaweza kuwaona tena.

Na ingawa hilo limeniumiza sana, sijutii chochote.

Wazazi wangu

Na baba yangu, Katika filamu hiyohiyo alikiri kwamba hakujua kilichokuwa kikiendelea Korea Kaskazini alipowatuma watoto wake kama zawadi.

Na ingawa hakuacha kuwa mwaminifu kwa chama cha serikali, maneno hayo yalimgharimu sana.

Watu wengi walimwona kuwa msaliti. Tayari amekufa na alipokuwa kwenye kitanda chake cha mauti, watu wengi walikuja kumwambia mama yangu kwamba mumewe alikuwa amesaliti chama.

m

Chanzo cha picha, Getty Images

Watu wachache sana walikuja kwenye mazishi yake.

Lakini katika yote hayo, mama yangu hakuwahi kuniambia niache nilichokuwa nikifanya. Daima alikuwa shabiki wa kazi yangu.

Mbele ya wengine, aliendelea kuwa vile vile. Lakini aliniambia faraghani kwamba haijalishi yuko Korea Kusini au Korea Kaskazini, jambo la muhimu ni kwamba anaishi kwa uhuru.

Alifariki hivi karibuni Na ninahisi kama hatimaye niliweza kusamehe kila kitu kilichotokea katika familia yetu.

Nilikasirika sana kwa muda mrefu. Nikijiuliza mambo mengi, "kwa nini walifanya hivyo? Kwa nini waliwapeleka mahali pale");