Video za mapishi ya kuchanganya 'mate' na 'mkojo 'katika chakula zaibua ghadhabu India

Chanzo cha picha, Getty Images
Na Srilan Mullen
BBC News
Baada ya video zinazoonyesha 'mate', 'mkojo' na uchafu vikichanganywa katika chakula na vinywaji kujitokeza, zimezifanya serikali za majimbo mawili ya India, Uttarakhand na Uttar Pradesh, kuanzisha sheria za utozaji faini kubwa na hukumu kali za jela dhidi ya wale waliopatikana na hatia miongoni watu wanaotengeneza chakula na vinywaji hivyo.
Jimbo la kaskazini la Uttarakhand linapanga kuweka faini ya hadi laki moja kwa wakiukaji wa sheria hiyo huku wakati jimbo jirani ya Uttar Pradesh likifikiria kuanzisha sheria kali kukabiliana na tatizo hilo.
Maagizo hayo ya serikali yamekuja baada ya video ambazo hazijathibitishwa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha wapishi katika vibanda na migahawa wakitema mate kwenye chakula wakati kinaandaliwa, na katika video moja, mjakazi wa nyumbani anaonekana akichanganya mkojo katika chakula anachokiandaa.
Jumapili, Waziri Mkuu wa Uttar Pradesh, jimbo kubwa zaidi nchini India, alitoa amri kama hiyo kwenye maduka, akidai kuwa ilikuwa na lengo la kuzuia ‘uchafuzi wa chakula', lakini wanaharakati wa kijamii na kisiasa wanasema, uamuzi huo unaweza kuwa na athari kubwa.
Amri hiyo inasema kwamba 'wachuuzi wote wanaouza bidhaa za chakula lazima waonyeshe jina na anwani ya waendeshaji, wamiliki na mameneja katika vituo vyao vya chakula.'
Baada ya video hizo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, watu wameelezea hasira zao juu ya hilo. Watu wengi wameelezea wasiwasi kuhusu usalama wa chakula katika majimbo hayo. Hata hivyo, baadhi ya video zinatajwa kama kampeni ya kuwalenga Waislamu na kuwalaumu. Baada ya uchunguzi wa kina wa video madai haya yamepingwa.
Watu wengi katika mitandao ya kijamii walidai kuwa mwanamke aliyeongeza mkojo kwenye chakula hicho alikuwa Muislamu, lakini baada ya kuchunguza ukweli huo, ilibainika kuwa mwanamke huyo alikuwa Mhindu.
Maafisa wanasema sheria hizo ngumu ni muhimu na zinalenga kuzuia ‘uchafuzi wa chakula’, lakini viongozi wa upinzani na wataalamu wa sheria wamehoji ufanisi wa sheria hizo, wakidai kuwa zinaweza pia kutumiwa vibaya kuchafua jamii fulani.
Gazeti la India Express ambalo ni gazeti kubwa la lugha ya Kiingereza nchini India, limekosoa pendekezo la sheria hiyo ya jimbo la Uttar Pradesh, likisema "itachochea ghasia za kijamii na uwezekano wa kuwalenga watu wachache ambao tayari wako katika mazingira magumu.
Usalama wa chakula pia ni suala la kisheria nchini India. Kwa mujibu wa mamlaka ya usalama wa chakula na viwango (FSSAI), chakula kisicho salama husababisha maambukizi ya takriban watu milioni 60 na vifo 400,000 kila mwaka nchini India.
Wataalamu nchini India wanataja sababu mbalimbali za ukosefu wa ubora wa viwango vya chakula, ikiwa ni pamoja na utekelezaji duni wa sheria za ubora wa chakula na ukosefu wa ufahamu. Majiko yaliyoharibika, sahani chafu, maji machafu, na usafirishaji wa vyombo usiofaa na mazoea ya kuhifadhi kwa muda mrefu chakula huongeza wasiwasi wa ubora wa chakula.
Kwa hivyo, wakati video za wauzaji wa migahawa wakitema mate katika chakula zilijitokeza, watu hawakushtushwa na tukio hilo tu bali walikasirika. Muda mfupi baadaye, jimbo la Uttarakhand lilitangaza faini kubwa kwa wale wanaofanya hivyo na kuwaagiza polisi kuwathibitisha wafanyakazi wa hoteli na kuhakikisha kila jiko la mgahawa na hoteli linakuwa na kamera za CCTV.
Katika jimbo la Uttar Pradesh, Waziri mkuu Yogi Adityanath alisema ili kuzuia matukio kama hayo kutokea tena, polisi wanapaswa kuthibitisha utambulisho wa kila mfanyakazi anayefanya kazi katika maduka na migahawa hii.
Jimbo hilo pia linapanga kufanya iwe lazima kwa vituo vya chakula kufichua majina ya wamiliki wao, kuhakikisha kuwa wapishi na wahudumu wanavaa barakoa na glavu, pamoja na kufunga kamera za CCTV katika hoteli na migahawa. .
Kwa mujibu wa ripoti, jimbo la Adityanath linapanga kuanzisha sheria mbili ambazo zitawezesha kutolewa kifungo cha mika hadi 10 jela kwa mtu atakayebainika kutemea mate chakula.

Chanzo cha picha, Amit Saini
Mnamo mwezi Julai, mahakama kuu ya India ilikataa utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na serikali za Uttarakhand na Uttar Pradesh, yaliyosema kuwa mahujaji katika tamasha la kila mwaka la kidini la Hindu 'Kanwar Yatra' Maduka yote yanayouza chakula na vinywaji lazima yaonyeshe jina na anwani ya waendeshaji wa biashara, wamiliki na mameneja katika vituo vyao vya chakula.
Walalamikaji waliiambia mahakama kuu kwamba miongozo hiyo iliwalenga Waislamu na itaathiri vibaya biashara zao.
Katika barua hiyo ambayo jopo la majaji wawili linalojumuisha Jaji Rishi Kesh Roy na Jaji SVN Bhatti wa mahakama kuu waliandika katika amri yao kuhusu maagizo yaliyotolewa na serikali za Uttarakhand na Uttar Pradesh kwamba 'wauzaji wa vyakula wanatakiwa kuandika aina ya chakula wanachouza lakini hawawezi kulazimishwa kuandika majina yao au majina ya wafanyakazi wao nje ya maduka.' [ya chakula].
Siku ya Jumatano, polisi katika mji wa Barkanki nchini humo walimkamata mmiliki wa mgahawa huo Mohammad Irshad kwa madai ya kutema mate wakati alipokuwa akiandaa mkate. Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Hindustan Times, Irshad ameshutumiwa kwa kuvuruga amani na maelewano ya kidini.
Mapema mwezi huu, polisi katika eneo la Uttarakhand la Mussoorie waliwakamata wanaume wawili, Naushad Ali na Hasan Ali, kwa kutema mate kwenye kijiko cha chai na walituhumiwa kuhatarisha afya ya umma.
Siku chache kabla ya kukamatwa kwa watu hao, video za wanaume hao waliokuwa wakitema mate kwenye mitandao ya kijamii zilipewa rangi ya kidini wakati akaunti nyingi za kizalendo za Kihindu zilipoanza kulielezea kama tukio la 'Spit Jihad' au 'Spitting Jihad' (Tema jihad).
Neno hilo linatokana na 'jihadi ya mapenzi', iliyoundwa na makundi ya Wahindu wenye msimamo mkali, ambao hutumia kuwashutumu wanaume wa Kiislamu kwa kuwabadilisha dini wanawake wa Kihindu kupitia ndoa. Zaidi ya hayo, baada ya 'Spitting Jihad', Waislamu wamekuwa wakishutumiwa kwa kujaribu kuwachafua Wahindu kwa kutema mate katika chakula chao.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hii si mara ya kwanza kwa Waislamu kukabiliwa na shutuma za kutemea mate chakula.
Wakati wa janga la Corona, mfululizo kama huo wa video bandia ulionekana kwenye mitandao ya kijamii ukiwaonyesha Waislamu wakitema mate, kupiga chafya au kulamba vitu ili kuwaambukiza watu virusi vya corona.
Video hizi zilichochea chuki za kidini na akaunti za Wahindu wenye msimamo mkali zilichangia kuchochea matamshi ya chuki dhidi ya Waislamu.
Viongozi wa upinzani katika jimbo la kaskazini linalotawaliwa na chama cha BJP nchini India la Uttarakhand na jimbo jirani la Uttar Pradesh wamekosoa miongozo hiyo mpya, wakisema inaweza kutumika kuwalenga Waislamu na kwamba serikali itatumia amri hizo ili kuondoa tahadhari za masuala mengine makubwa kama ukosefu wa ajira na kupanda kwa mfumuko wa bei.
Lakini afisa wa usalama wa chakula wa Uttarakhand Manish Sayana anasema maagizo ya serikali yanalenga tu kuboresha ubora wa chakula na usalama.
Aliiambia BBC kwamba maafisa wa usalama wa chakula na polisi walianza kukagua maduka ya chakula na walikuwa wakijaribu kuhakikisha wanavaa barakoa na glavu na kuweka kamera za CCTV.
Mtaalamu wa sheria na mwandishi wa habari V Venkatesan anasema kwamba sheria mpya na sheria nyingine zinazohusiana na usalama wa chakula zinahitaji kujadiliwa katika mkutano.
"Kulingana na mimi, sheria zilizopo (chini ya sheria ya usalama wa chakula na viwango, ya 2006) zinatosha kwa usalama wa chakula, kwa hivyo kuna haja gani ya sheria mpya na miongozo wakati kuna sheria");