Jinsi madaktari wa kike wa upasuaji walivyonyanyaswa kingono wakati wa upasuaji

Chanzo cha picha, Getty Images
Madaktari wa upasuaji wa kike wanasema wananyanyaswa kingono, kushambuliwa na katika visa vingine kubakwa na wenzao, uchambuzi mkubwa wa wafanyakazi wa Huduma ya afya ya Uingereza -NHS umegundua.
BBC News imezungumza na wanawake ambao walinyanyaswa kingono katika chumba cha upasuaji wakati upasuaji ukifanyika.
Waandishi wa utafiti huo wanasema kuna mtindo wa wanafunzi wa kike kudhalilishwa na madaktari bingwa wa upasuaji wa kiume, na hii inafanyika sasa, katika hospitali za NHS.
Chuo cha Royal cha Madaktari wa upasuaji kilisema matokeo hayo "yalishtua sana".
Unyanyasaji wa kijinsia, unyanyasaji wa kingono na na ubakaji vimetajwa kuwa siri ya wazi ya upasuaji.
Kuna hadithi ambayo haijaelezewa ya wanawake ambapo wapasuaji wa kiume waliwatomasa na kugusisha sehemu za siri kwenye miili ya wafanyakazi wa kike. Wengine wamejitoa kingono ili kupata fursa za kazi.
Uchambuzi wa Chuo Kikuu cha Exeter, Chuo Kikuu cha Surrey na kitengo cha kinachoshughulikia Utovu wa Kimapenzi katika Upasuaji – vimefanya mahojiano ya kipekee na na BBC News.
Takriban theluthi mbili ya madaktari wa upasuaji wa wanawake waliojibu watafiti hao walisema wamekuwa walengwa wa unyanyasaji wa kijinsia na theluthi moja wamedhulumiwa kingono na wenzao katika miaka mitano iliyopita.
Wanawake wanasema wanahofia kuwa kuripoti matukio kutaharibu kazi zao na hawana imani kuwa NHS itachukua hatua.