Malawi: Kundi la WhatsApp lilivyowaokoa wanawake waliosafirishwa kwenda Oman

fdcv

Chanzo cha picha, Florence Phiri/BBC

  • Author, Florence Phiri & Tamasin Ford
  • Nafasi, BBC Africa Eye

BBC Africa Eye imechunguza jinsi kikundi cha WhatsApp kilivyosaidia kuokoa zaidi ya wanawake 50 wa Malawi waliosafirishwa hadi Oman kufanya kazi katika mazingira kama ya watumwa.

Onyo: Baadhi ya maelezo katika makala hii ni ya kuhuzunisha.

Mwanamke mwenye umri wa miaka 32 anaangua kilio anapokumbuka unyanyasaji alioupata wakati akitarajia maisha bora. Alijikuta akifanya kazi za ndani nchini Oman.

Georgina, na wanawake wengine waliosafirishwa kwa njia haramu walihojiwa na BBC, aliamini ameajiriwa kufanya kazi ya udereva huko Dubai.

Alikuwa akifanya biashara ndogo ndogo mjini Lilongwe, mji mkuu wa Malawi, alipofuatwa na wakala akisema atapata pesa nyingi zaidi Mashariki ya Kati.

Ndege ilipotua Muscat, mji mkuu wa Oman, ndipo alipogundua amedanganywa na hatimaye kuingia katika familia ambayo ilimfanya afanye kazi kwa saa nyingi, siku saba kwa wiki.

"Nilifikia hatua ambayo sikuweza kuvumilia," anasema, akielezea jinsi alivyo lala saa mbili.

Muda si mrefu na bosi wake akaanza kumlazimisha kufanya naye ngono, akitishia kumpiga risasi ikiwa angesema chochote.

"Si yeye tu," anasema. "Alileta marafiki, ambao walimlipa bosi huyo."

Anasimulia kwa tabu jinsi alivyolazimishwa kufanya ngono kinyume na maumbile. "Nilijeruhiwa vibaya sana. Nilikuwa na hofu sana."

Pia unaweza kusoma

Takwimu Zinatisha

Inakadiriwa kuwa kuna wafanyakazi wa nyumbani wapatao milioni mbili katika mataifa ya Ghuba ya Kiarabu.

Katika uchunguzi wa wanawake 400 nchini Oman uliofanywa na shirika la misaada la wahamiaji la Do Bold, uliochapishwa 2023, karibu wote walikuwa wahanga wa biashara haramu ya binadamu.

Takribani thuluthi moja walisema walinyanyaswa kingono, huku nusu wakiripoti unyanyasaji wa kimwili na ubaguzi.

Baada ya wiki kadhaa, Georgina alikata tamaa na akaweka chapisho kwenye Facebook kuomba mtu amsaidie.

Maelfu ya maili katika jimbo la New Hampshire nchini Marekani, mwanaharakati wa mtandao wa kijamii wa Malawi Pililani Mombe Nyoni mwenye umri wa miaka 38 aliona ujumbe wake na akaanza kuchunguza.

Alifanya mawasiliano na ujumbe huo ukaondolewa Facebook kwa usalama wa Georgina na kuweka namba yake ya WhatsApp ambayo ilianza kusambaa nchini Oman. Ndipo aligundua tatizo ni kubwa sana.

"Georgina alikuwa mwathirika wa kwanza. Kisha wakawa wawili, kisha watatu," aliambia BBC.

"Hapo ndipo niliposema: 'Nitaunda kikundi cha [WhatsApp] kwa sababu hii inaonekana kama biashara ya binadamu."

Zaidi ya wanawake 50 wa Malawi wanaofanya kazi kama wafanyakazi wa nyumbani nchini Oman walijiunga na kikundi hicho.

Punde kundi hilo la WhatsApp lilijaa sauti na video, zingine zikiwa za kuhuzunisha sana kutazama, zikielezea hali ya kutisha ambayo wanawake hao walikuwa wakipitia. Wengi wao pasipoti zao zilichukuliwa mara tu walipofika, na kuzuiwa kuondoka.

Wengine walisimulia jinsi walivyojifungia kwenye vyoo ili kutuma jumbe zao kwa siri na jumbe za kuomba msaada.

"Ninahisi kama niko gerezani ... hatuwezi kamwe kutoroka," mmoja alisema.

"Maisha yangu yako hatarini," mwingine alisema.

FV

Chanzo cha picha, Florence Phiri/BBC

Maelezo ya picha, Katika uwanja wa ndege wa Lilongwe, Blessings akikumbatiana na familia yake Oktoba mwaka jana

Nyoni alianza kuzungumza na mashirika nchini Malawi na akatambulishwa kwa Ekaterina Porras Sivolobova, mwanzilishi wa Do Bold, iliyoko Ugiriki.

Do Bold hufanya kazi na jumuiya ya wafanyakazi wahamiaji katika nchi za Ghuba, kuwatambua waathiriwa wa biashara haramu ya binadamu au kazi za kulazimishwa na kisha kujadiliana na mwajiri wao ili waachiliwe.

"Mojawapo ya changamoto zinazotukabili ni kwamba mwajiri au wakala anasema: 'Nataka pesa zangu zirudi, kisha ndipo arudi nyumbani'," Bi Sivolobova aliambia BBC.

"Sheria zilizopo [nchini Oman] zinakataza mfanyakazi wa ndani kuondoka kwa mwajiri wake. Hawezi kubadilisha kazi na hawezi kuondoka nchini - bila kujali jinsi unavyotendewa."

Mtindo huu unajulikana Mashariki ya Kati kama mfumo wa kazi wa "kafala," ambapo wafanyakazi na waajiri wao huwa wote kwa muda wote wa mkataba.

Kamati ya Kitaifa ya Oman ya Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu iliiambia BBC, mkataba kati ya mwajiri na mfanyakazi wa ndani ni wa makubaliano ya pande mbili - na mizozo kati yao inaweza kuwasilishwa katika mahakama ndani ya wiki moja.

Iliongeza kuwa mwajiri haruhusiwi "kumlazimisha mwajiriwa kufanya kazi ya aina yoyote" na hatakiwi kuishikilia "pasipoti na nyaraka binafsi za mfanyakazi bila idhini ya maandishi."

Baada ya miezi mitatu na kwa usaidizi wa Nyoni na mtu mwingine huko Oman, Georgina alirejea Malawi mwezi Juni 2021.

“Baada ya kumsaidia Georgina, nilihisi hasira sana,” anasema Nyoni.

Wanawake wengine

Kesi ya Georgina ilimruhusu kupaza sauti ndani ya Malawi - na shinikizo lilianza kuongezeka kwa serikali kuingilia kati.

Kituo cha misaada cha Malawi cha Demokrasia na Mipango ya Maendeleo ya Kiuchumi (CDEDI) kilizindua kampeni ya uokoaji ya Oman, na kutoa wito kwa mamlaka kuwarudisha nyumbani wanawake hao.

Baraka alikuwa mwanamke mwingine katika kundi la WhatsApp. Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 39 alisafiri hadi Muscat mnamo Desemba 2022, akiwaacha watoto wake wanne na dada yake, Stevelia, huko Lilongwe.

Aliungua moto katika jiko la nyumba aliyokuwa akifanya kazi, lakini mwajiri wake hakumruhusu kurudi Malawi.

"Kiwango cha majeraha ni kikubwa, niamini, nilihisi dada yangu atapoteza maisha," Stevelia aliambia BBC.

"Nakumbuka dada yangu alisema: 'Dada, nilikuja hapa kwa sababu nilihitaji maisha bora, lakini nikifa, tafadhali watunze watoto wangu.' Hilo liliniumiza.

FVC

Chanzo cha picha, Florence Phiri/BBC

Maelezo ya picha, Georgina anapata utulivu akibarizi Ziwa Malawi

Stevelia alianza kushawishi dada yake arejeshwe nyumbani. Mwanzoni wakala huyo aliiambia familia kwa hasira kwamba Blessings amekufa, lakini haikuwa kweli na hatimaye alirejea Oktoba mwaka jana, kwa msaada wa serikali ya Malawi.

"Sikuwahi kufikiria kuwa – ningeweza kuiona familia yangu tena, watoto wangu," Blessings aliambia BBC.

"Sikujua kuna watu duniani ambao wanawatendea wengine kama watumwa."

Serikali ya Malawi, ambayo pia ilifanya kazi na Do Bold, inasema imetumia zaidi ya dola za kimarekani 160,000 kuwarejesha wanawake 54 kutoka Oman.

Lakini Aida Chiwalo mwenye umri wa miaka 23 alirejea nyumbani akiwa ndani ya jeneza. Hakukuwa na uchunguzi wa maiti au uchunguzi uliofanyika nchini Oman baada ya kifo chake.

Mamlaka ya Oman ilisema wizara ya kazi haijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wafanyakazi wa nyumbani wa raia wa Malawi mwaka 2022 na kulikuwa na lalamiko moja tu mwaka 2023 ambalo lilitatuliwa.

“Wengi wa wanawake hawa wameachiliwa kwa sababu waajiri wamelipwa, kutoka dola 1,000 hadi 2,000,” anasema Sivolobova.

"Kwa hiyo kimsingi, uhuru wao ulipaswa kununuliwa. Na hilo ndilo linalonisumbua. Unawezaje kununua uhuru wa mtu mwingine");