Makosa 13 ya VAR kwenye ligi ya Premier kufikia sasa msimu huu

Chanzo cha picha, Getty Images
Kumekuwa na makosa 13 ya waamuzi wasaidizi wa video (VAR) katika Ligi ya Premia hadi sasa msimu huu – yakiwa ya chini kutoka 20 yaliofanyika katika hatua sawa muhula uliopita - kulingana na wakuu wa ligi.
Hatua nne zisizo sahihi za VAR na uingiliaji kati mara tisa uliofanyika kimakosa kutoka kwa mzunguko wa mechi za kwanza 23 zimegunduliwa na jopo la Matukio Muhimu ya Mashindano (KMI).
Kumekuwa na uingiliaji kati mara 70 wa VAR katika mechi 239 za ligi msimu huu - karibu moja katika kila mechi tatu.
Ligi hiyo inasema usahihi wa 'Matukio Muhimu ya Mechi' ni 96.4% - kutoka 95.7% katika hatua inayolingana muhula uliopita.
"Hakuna mtu anayedharau umuhimu na athari ya kosa moja," afisa mkuu wa kandanda Tony Scholes alisema.
"Tunajua kwamba kosa moja linaweza kugharimu klabu. Pointi na matokeo yanaweza kuathiri nafasi za wasimamizi, na nafasi za wachezaji ."
Katika kesi ya Erik ten Hag, hilo ndilo lililotokea - moja ya makosa manne ilikuwa adhabu iliyotolewa dhidi ya timu yake ya Manchester United katika mechi ambayo ilionekana kuwa mechi yake ya mwisho.
Waamuzi pia wamekuwa wakidhulumiwa, huku polisi hivi majuzi wakichunguza "vitisho na unyanyasaji" uliyoelekezwa kwa Michael Oliver kufuatia ushindi wa Arsenal wa 1-0 dhidi ya Wolves mnamo Januari.
Oliver kwa utata alimtoa kwa kadi nyekundu beki wa Gunners Myles Lewis-Skelly - uamuzi ambao ulibatilishwa baada ya kukata rufaa.
Aliyekuwa mwamuzi David Coote alifutwa kazi na bodi ya waamuzi mwezi Disemba baada ya "uchunguzi wa kina" kuhusu mwenendo wake.
Alipoulizwa kuhusu imani kwa viongozi, Scholes alisema: "Sote tuna jukumu la kuwa na usawa katika maoni ambayo yanatolewa.
"Hatuwezi kuwa na viongozi, sehemu muhimu ya ligi yenye mafanikio na burudani, inayokabiliwa na aina ya unyanyasaji unaotokea mara kwa mara.
"Watu hawa ni wazuri. Najua huo sio mtazamo kila wakati, lakini ulimwengu wote unatambua jinsi walivyo wazuri."
Ligi ya Premia ilikataa kuorodhesha hatua tisa zenye makosa - na iwapo hatua hizo ni pamoja na kadi nyekundu ya Lewis-Skelly. Ilielezea makosa manne kwa vyombo vya habari.
Makosa manne ya VAR yalikuwa yapi?
Outtara 'aliunawa mpira' - Bournemouth 1-1 Newcastle, 25 Agosti
Nini kilichotokea: Dango Outtara alidhani aliifungia Bournemouth bao la ushindi dakika za lala salama aliporuka na kuupiga mpira kwa kichwa. Bao hilo lilikubaliwa na mwamuzi wa uwanjani David Coote.
Uamuzi: Mwamuzi msaidizi wa VAR Tim Robinson alimshauri Coote kutengua uamuzi wake, akiona kuwa ni mpira ulioshikwa na mkono. Hakumsisitizia mwamuzi Coote kwenda kufuatilia kwenye runinga.
Matokeo: Bila ushahidi wa kutosha kwamba mpira ulikuwa chini ya mkono wa Ouattara na kuuona kama mpira ulioshikwa, mkuu wa PGMOL Howard Webb - akizungumza kwenye Maafisa wa Mechi ya Sky Sports Mic'd Up - alisema VAR haikuwa sahihi kuingilia kati.
De Ligt alimfanyia madhambi Ings - West Ham 2-1 Man Utd, 27 Oktoba
Nini kilichotokea: Mshambulizi wa West Ham Danny Ings alianguka ndani ya eneo la hatari huku akipigania mpira na beki wa Manchester United Mathijs de Ligt. Mwamuzi David Coote alisema mchezo uendelee lakini akashauriwa na mwamuzi msaidizi wa VAR Michael Oliver kukagua tukio hilo kwenye runinga iliopo uwanjani.
Uamuzi: Coote alitoa penalti, ambayo Jarrod Bowen alifunga na kuipa ushindi West Ham.
Matokeo: Meneja wa Man Utd aliyekuwa na presha Ten Hag alifutwa kazi siku iliyofuata. Webb baadaye alisema The Hammers hawakupaswa kupewa penalti.
Kadi nyekundu ya Norgaard - Brentford 0-0 Everton, 23 Novemba
Nini kilichotokea: Christian Norgaard wa Brentford alimgusa goti mlinda lango wa Everton Jordan Pickford wakati akigombea mpira kwenye eneo la hatari.
Uamuzi: Mwamuzi Chris Kavanagh hakuchukua hatua lakini alishauriwa na VAR kuchunguza tukio hilo. Baadaye alimuonyesha Norgaard kadi nyekundu ya moja kwa moja.
Matokeo: Kusimamishwa kwa Norgaard kwa mechi tatu kwa kucheza vibaya kulibatilishwa na jopo huru kufuatia rufaa
Bao la Milenkovic lilikataliwa - Nottingham Forest 3-2 Southampton, 19 Januari
Nini kilichotokea: Nikola Milenkovic alifunga bao la kichwa na kuifanya Nottingham Forest kuwa mbele kwa mabao 4-1.
Uamuzi: VAR ilimshauri mwamuzi Anthony Taylor kukataa bao hilo huku mshambuliaji wa Forest Chris Wood akitoka katika nafasi ya kuotea na kuwazuia mabeki wa Southampton kugombea mpira. Wood hakuugusa mpira.
Matokeo: Jopo huru liligundua kwamba bao hilo lingekubaliwa
'Hatua kubwa' imepigwa kwenye teknolojia ya kuotea
Ilitarajiwa teknolojia ya kuotea ambayo hutumiwa katika mashindano ya Fifa na Uefa, ingeanzishwa katika madirisha ya kimataifa ya Oktoba au Novemba.
Maafisa wa ligi wanatumai itapunguza muda unaochukuliwa wa kuangalia wachezaji waliootea kwa sekunde 31.
Scholes, licha ya mashaka yaliotokea, anasema kumekuwa na maendeleo makubwa katika kipindi cha "wiki nne hadi sita", na nia bado ni kuitumia msimu huu.
"Teknolojia hii haiboreshi usahihi, inafanya mchakato kuwa mzuri zaidi," alisema.
"Kwa nini usiitambulishe ikiwa una uhakika kabisa iko tayari");