Waridi wa BBC: 'Saratani si hukumu ya kifo'

Chanzo cha picha, Annah Kilawe, IG
- Author, Esther Namuhisa
- Nafasi, BBC News Dar es Salaam
- Twitter,
Ugonjwa wa saratani ni miongoni mwa magonjwa yanayoleta madhara makubwa kiafya na hata kusababisha vifo kwa mamilioni ya watu ulimwenguni. Kwa wengi, kugundulika na saratani ni kama hukumu ya kifo, lakini kwa Annah Kilawe, ilikuwa mwanzo wa safari yenye changamoto, matumaini, na hatimaye ushindi mkubwa dhidi ya ugonjwa huu.
Annah alikuwa msichana wa miaka 17 mwenye ndoto na maisha yaliyojaa matumaini. Hakuwa na wazo lolote kwamba maisha yake yangepitia mabadiliko makubwa kiasi cha kumlazimu kufanya maamuzi magumu ili aendelee kuishi.
Mnamo, mwaka 2020, Annah alianza kupata maumivu ya mgongo na kiuno. Alijihisi mchovu sana, hali iliyomfanya aonekane mvivu kwa macho ya familia yake. Awali, alihisi huenda ni uchovu wa kawaida, lakini hali ilipozidi kuwa mbaya, aliamua kutafuta msaada wa kitabibu.

Alikwenda hospitalini kwa mara ya kwanza, ambapo alielekezwa kufanya mazoezi ili kupunguza maumivu. Lakini kila alipomaliza mazoezi, hali ilikuwa inazidi kuwa mbaya. Baadaye, aliporejea shuleni Biharamulo, baba yake aliwataarifu walimu wake kuhusu hali yake, wakiamini angepata uangalizi wa karibu.
Hata hivyo, mwezi mmoja baadaye, hali ilizidi kuwa mbaya. Alipatwa na homa kali, jambo lililomfanya kurudi nyumbani kwa uchunguzi zaidi. Hatimaye, alifikishwa hospitali ya taifa, jijini Dar es salaam, Muhimbili kwa uchunguzi wa kina, alielezwa kuwa matatizo yake yalihusiana na kiuno na kwamba baada ya wiki moja angeruhusiwa kurudi nyumbani.
Saratani na Uamuzi Mgumu

Chanzo cha picha, Annah IG
Siku ya kuchukua majibu ya vipimo ilipowadia, Annah alifuatana na baba yake hospitalini. Alishangaa jinsi baba yake alivyobadilika ghafla na alikuwa mpole kupita kawaida, akimfurahisha na kumnunulia chakula cha gharama kubwa. Lakini Annah hakuwa na hamu ya kula.
Walipofika nyumbani, baba yake aliagiza apewe kila kitu anachotaka na asifanye kazi yoyote. Annah alianza kushuku kuna jambo kubwa linajificha. Siku iliyofuata, alikwenda hospitali na mama yake. Aliona wazazi wake wakiwa karibu sana, hali iliyokuwa tofauti na kawaida yao maana walikuwa hawaishi wote.
Alipowauliza kulikoni, walimwambia kila kitu kitakuwa sawa. Ukweli ni kwamba, madaktari waliwaambia wazazi wake kuwa Annah alikuwa na saratani ya nadra iitwayo Rhabdomyosarcoma, ambayo hushambulia tishu laini za mwili. Zaidi ya hapo, waliambiwa kuwa hata akifanyiwa upasuaji wa kukata mguu, nafasi yake ya kuishi alipewa miezi minne tu ya kuishi, akikatwa au asipokatwa mguu.
Ilipofika usiku wa siku hiyo ya majibu akiwa nyumbani, Annah alisikia mama yake akilia wakati akiongea na simu, akitaja suala la miezi minne. Alishtuka na kumuuliza mama yake, "Kwa hiyo mimi nitakufa");