Matumaini na mashaka: Mashariki ya Kati ikisubiri kurejea kwa Trump

Chanzo cha picha, Frank Gardner
- Author, Frank Gardner
- Nafasi, BBC News World
Wakati viongozi wa mataifa kadhaa ya Kiarabu na Kiislamu wakikusanyika katika mji mkuu wa Saudia kwa mkutano wa kilele, kuna swali juu ya muhula wa pili wa Trump kwa eneo hilo.
Kinyume kabisa na hofu iliyopo barani Ulaya kuhusu kutotabirika kwa Donald Trump, nchi za Kiarabu za Ghuba zinamwona kama nguvu ya utulivu.
Katika makala yake ndani ya Arab News, mfanyabiashara mashuhuri wa UAE, Khalaf al-Habtoor anasema: "Mashariki ya Kati ambako usalama ni muhimu, mtazamo wa Trump wa kuimarisha miungano na kuzuia vikundi vya itikadi kali – ni mtazamo mzuri."
Hapa Saudi Arabia, Trump anatazamwa vyema zaidi kuliko Joe Biden.
Trump alikwenda Riyadh kwa safari yake yake ya kwanza nje ya nchi kama Rais mwaka 2017, wazo linaloelezwa ni kutoka kwa Rupert Murdoch.
Kupitia mkwe wake Jared Kushner, Trump anafurahia mahusiano mazuri na mtawala wa Saudia, Mwanamfalme Mohammed bin Salman. Mwanamfalme huyo hajawahi kusamehe au kumsahau Biden pale aliposema Saudi Arabia inapaswa kutengwa kwa kukiuka haki za binadamu.