Afghanistan: Vilio na maandamano huku Taliban ikifunga vyuo vikuu kwa wanawake

m

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wanafunzi wa kike wa chuo kikuu walisimamishwa kutoingia ndani ya chuo na maafisa wa usalama wa Taliban huko Kabul siku ya Jumatano

Ni agizo ambalo wasichana na wanawake wa Afghanistan wamekuwa wakiogopa tangu Wataliban waliporejea. Siku ya Jumatano, wasichana waliovalia hijabu walifika kwenye maeneo yao ya chuo kikuu ila wakazuiwa na walinzi wa Taliban.

 Kanda za video zinaonesha wasichana hao katika makundi wakilia huku wakifukuzwa.

 Baada ya kuwazuia wasichana wasisome katika shule nyingi za sekondari kwa miezi 16 iliyopita, wiki hii pia Taliban ilipiga marufuku elimu ya chuo kikuu kwa wanawake.

"Wameharibu daraja pekee ambalo linaweza kuniunganisha na maisha yangu ya baadaye," mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Kabul aliambia BBC.

"Ninawezaje kukabiliana na hili? Niliamini kwamba ningeweza kusoma na kubadili maisha yangu ya baadaye au kuleta mwanga kwenye maisha yangu lakini wameharibu."

Mamlaka zilitoa agizo hilo siku ya Jumanne - na kufikia siku iliyofuata maeneo mengine ya kusomea, ikiwa ni pamoja na shule za dini ya Kiislamu na vyuo vya kibinafsi katika majimbo kadhaa, pia yalikuwa yakitekeleza uamuzi huo. 

Vyanzo kutoka majimbo matatu - Takhar kaskazini, Ghazni kusini-mashariki na mji mkuu Kabul - vilithibitishia BBC kwamba Taliban imewazuia wasichana kuhudhuria vituo vya elimu ya kibinafsi.

Njia zote za elimu rasmi kwa wanawake zinafungwa, inaonekana.

Ilipelekea baadhi ya wanawake kuthubutu kuandamana siku ya Jumatano mitaani mjini Kabul - kitendo cha hatari kutokana na rekodi ya Taliban ya kuwaweka kizuizini waandamanaji. Maandamano hayo madogo yalifungwa haraka na maafisa wa Taliban.

Kizazi hiki kilifikiri wao ndio waliobahatika - kupata elimu iliyonyimwa kwa mama zao, dada zao wakubwa na binamu zao.

Badala yake, wanaona maisha yao ya baadaye yanaharibika.

Unaweza pia kusoma
m

Kundi la Taliban, ambalo lilianza kama kundi la wapiganaji wa Kiislamu lenye msimamo mkali, liliahidi kuheshimu haki za wanawake waliporejea madarakani mwezi Agosti mwaka jana - baada ya kusitisha utawala uliokuepo, wao awali walitawala kutoka mwaka 1996-2001 wakati wanawake hawakuweza kufanya kazi au kusoma.

 Lakini amri yao ya hivi karibuni inaondoa uhuru na haki ndogo zozote walizopewa wanawake baada ya majeshi yanayoongozwa na Marekani kuondoka Afghanistan na Taliban kurejea.

Hata hivyo miezi mitatu tu iliyopita, Taliban walikuwa wamekubali kuruhusu mitihani ya kujiunga na chuo kikuu kuendelea.

 Maelfu ya wasichana na wanawake walifanya majaribio katika majimbo kote nchini. Wengi walikuwa wamesoma kwa siri - nyumbani au kuhatarisha kujitosa kwenye vyuo vya ualimu vilivyofichwa vilivyowekwa kwa ajili ya wasichana.

 Hatari ilikuwepo kila wakati. Wakati baadhi ya mitihani washambuliaji walilenga shule na kuua wanafunzi.

Lakini bado wasichana waliendelea kusoma.

 Hata wakati Taliban mwezi Novemba walipoleta vikwazo vya dakika za mwisho kwa masomo - kuwazuia wasichana kutoka katika masomo kama vile uchumi, uhandisi na uandishi wa habari - waliendelea kujaribu, wengi wakiomba kufundisha na udaktari.

Kama mwanafunzi mwingine wa kike alivyoiambia BBC: "Kwa nini tuwe wahanga kila wakati? Afghanistan ni nchi maskini. Lakini wanawake katika nchi hii wamekubali umaskini pamoja na kila tatizo lingine na bado wanapaswa kuteseka."

women

Chanzo cha picha, AFP

Masomo ya wasichana kwa muda mrefu yamekuwa suala la mzozo kati ya vikundi vya kihafidhina na vya wastani zaidi katika Taliban.

Marufuku ya chuo kikuu sasa yanaonesha ushindi wa mtu mwenye msimamo mkali zaidi katika Taliban, ambaye kiongozi wake mkuu Hibatullah Akhundzada anaamini kuwa elimu ya kisasa - hasa kwa wanawake na wasichana - sio sahihi katika mafundisho ya Kiislamu.

Hata hivyo si kila mtu katika chama tawala anafikiri kama yeye - na kulikuwa na ripoti zaidi ya maafisa wenye msimamo wa wastani katika miji kama vile Kabul walitaka wasichana wenye umri wa zaidi ya miaka 12 kupata elimu.

Kama watetezi wa haki wameonya, uamuzi huo una athari kwa mustakabali wa nchi nzima. "Hakuna nchi inayoweza kustawi wakati nusu ya wakazi wake wamezuiliwa," Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken alionya.

Nchi za Magharibi zilisisitiza juu ya elimu ya wanawake kama sharti ambalo Taliban wangehitaji kutimiza ikiwa wanataka kutambuliwa kimataifa. Hata hivyo Taliban wamepuuza ukosoaji huo hadi sasa.

 

Kwa familia za Afghanistan, ndani ya nchi na duniani kote, kuona mustakabali wa binti zao kurudi katika "zama za giza" kumezua hofu na hasira.

Habari za kupigwa marufuku kwa chuo kikuu zilisababisha baadhi ya wanaharakati wanawake wa Afghanistan kuchapisha hadithi za siku zao za kuhitimu chuo kikuu - wakiwa wamevalia kofia na majoho.

 Msukumo dhidi ya Taliban tangu wachukue mamlaka tena haujatosha, wanasema.

Na ni sehemu ya wimbi linaloongezeka la vizuizi kwa maisha ya kila siku ya wanawake katika wiki za hivi karibuni. Mnamo Novemba, wanawake huko Kabul pia walizuiwa kuingia katika maeneo ya umma kama vile bustani na ukumbi wa michezo. Wanawake wanazidi kuzuiliwa majumbani mwao katika sera sawa na kifungo, inasema UN.

m

Chanzo cha picha, Getty Images

'Matendo si ya Uislamu'

Kwa mwanafunzi mmoja wa sheria, elimu yake ya juu inaonekana imekwisha sasa. Muda wake wa chuo kikuu ulikuwa umeisha kwa mapumziko ya msimu wa baridi na haukutarajiwa kuanza tena hadi Machi.

Lakini sasa haruhusiwi kurudi chuo - "amepoteza kila kitu". Akiwa msomi wa sheria za Sharia, aliiambia BBC kuwa anajitahidi kuelewa jambo hilo kulingana na mafundisho ya Kiislamu.

"Taliban wamechukua haki ambazo Uislamu na Mwenyezi Mungu ametupa," aliiambia BBC.

"Lazima waende katika nchi nyingine za Kiislamu na kuona kwamba matendo yao si ya Kiislamu. Kulingana na wanachosema hii ni Sharia. Lakini kwa nini wanataka kuitekeleza kwa wanawake pekee? Kwa nini hawaitumii kwa wanaume");