'Haki za mtoto wangu ambaye hajazaliwa zinakiukwa'

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Leire Ventas
- Nafasi, BBC News Mundo, Los Angeles
- Twitter,
"Mtoto wangu hata hajaja katika ulimwengu huu, na haki zake tayari zinakiukwa," anasema Meya, akizungumza na BBC. Jina lake tumelibadilisha kutokana na kesi yake ya kisheria.
Ni mtafuta hifadhi kutoka Honduras anayeishi California tangu 2021, Meny anakabiliwa na hofu kama ilivyo kwa wahamiaji wengine Marekani, ambao hawana uhakika na hatima yao.
Amri iliyotiwa saini na Donald Trump siku ya kwanza ya urais wake, ina lengo la kuondosha uraia wa kuzaliwa. Uraia hutolewa moja kwa moja kwa mtu yeyote aliyezaliwa Marekani - kwa miaka 160 sasa. Lakini hilo huenda sasa likabadilika.
Trump anataka nini?

Chanzo cha picha, Reuters
Agizo la Trump linalenga kubadilisha sheria na kuwanyima uraia watoto wa wahamiaji ambao wapo Marekani kinyume cha sheria au kwa viza ya muda. Inawahusu watoto waliozaliwa tarehe 19 Februari na kuendelea, na haitatumika kwa watoto waliozaliwa kabla ya tarehe hii.
Zaidi ya nchi 30, hasa katika mabara ya Amerika, zinatoa haki ya utaifa au uraia kwa mtu yeyote aliyezaliwa katika nchi husika. Mataifa mengine, kama vile Uingereza na Australia, hutoa uraia ikiwa mzazi mmoja ni raia au mkazi wa kudumu.
Agizo la Trump limezua vita vya kisheria na kuziacha familia kama ya Meny katika hali ya wasiwasi na kuchanganyikiwa.
Majimbo 22 yanayoongozwa na chama cha Democratic, pamoja na jiji la San Francisco, Wilaya ya Columbia, na makundi ya haki za kiraia tayari yameishitaki serikali ya shirikisho na kupinga amri hiyo.
Amri hiyo ya rais ilipata pigo mapema katika siku ya nne ya urais, pale Jaji wa Mahakama ya Wilaya, John Coughenour alipoiita ni "kinyume cha katiba" na kutoa amri ya kuizuia kwa muda.
Kwa sasa imesitishwa kusubiri taratibu zaidi za kisheria lakini mawakili wa serikali ya shirikisho wanapanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, na wanatarajia kesi hiyo kufika mbele ya Mahakama ya Juu ya Marekani.
Sheria ya sasa ya uhamiaji
Trump kwa muda mrefu ameahidi kukomesha uraia wa kuzaliwa, huku watu wenye msimamo mkali dhidi ya uhamiaji wakisema, sheria ya sasa inawavutia wahamiaji haramu na inawafanya wajawazito wasio na vibali kuvuka mpaka ili kujifungua.
Kulingana na taasisi ya utafiti ya Washington, Pew Research, watoto 250,000 waliozaliwa mwaka 2016 walizaliwa na wazazi wahamiaji wasio na vibali halali vya kuishi Marekani.
Kufikia 2022, kuna raia milioni 1.2 wa Marekani waliozaliwa na wazazi wahamiaji ambao hawana vibali vya kuishi.
Kwa vile watoto hao pia nao watakuwa na watoto, athari ya kuzuia haki ya uraia wa kuzaliwa ifanya kuongezeka kwa idadi ya wahamiaji wasio na vibali hadi milioni 4.7 ifikapo mwaka 2050, inasema Taasisi ya fikra tunduizi kuhusu Sera za Uhamiaji.
Katika mahojiano na kipindi cha Meet the Press cha NBC, Trump amesema watoto wa wahamiaji wasio na vibali wanapaswa kufukuzwa pamoja na wazazi wao - hata kama walizaliwa Marekani.
"Sitaki kutenganisha familia," alisema Trump mwezi Disemba mwaka jana. "Kwa hivyo njia pekee ili nisitenganishe familia ni kuwaweka pamoja na lazima uwarudishe wote."
Vita vya kisheria

Chanzo cha picha, Getty Images
Wataalamu wanasema sheria ya sasa haiwezi kubadilishwa tu kwa amri ya rais, itahitaji marekebisho ya katiba – ni mchakato ambao unahitaji theluthi mbili ya kura katika mabaraza yote mawili ya Congress, pamoja na idhini ya majimbo ya Marekani. Wataalamu wanasema suala hilo litaamuliwa tu na mahakama.
Familia za wahamiaji zinasema wasiwasi wao umesababisha dhiki kubwa, zikihofia watoto wao watanyimwa haki ya kimsingi ya uraia ambayo imekuwepo kwa muda mrefu.
Meny anasema. "Nina imani hili halitafanikiwa. Lakini kuna hofu kuhusu kile ambacho kitatokea."
Kesi ya Meny ni mojawapo ya kesi nyingi zilizojumuishwa katika kesi iliyowasilishwa na Mradi wa Watetezi wa Watafuta Hifadhi (ASAP), shirika ambalo linawakilisha zaidi ya watu 650,000 wanaotafuta hifadhi.
"Tunataka amri ya rais itangazwe kuwa ni kinyume cha katiba na kinyume cha sheria," anasema wakili na msemaji wa ASAP, Leidy Pérez.
Anasema agizo la Trump limejaa maswali ambayo hayajapatiwa majibu. "Nini kitatokea kwa watoto watakaonyimwa uraia ambao wazazi wao ni watafuta hifadhi");