Jinsi kijiji kidogo kilivyogeuka kuwa mji mkuu wa YouTube

f

Chanzo cha picha, Estudio Santa Rita

  • Author, Saqib Mugloo
  • Nafasi, BBC

Tulsi, kijiji kilicho katikati mwa India, kimeibua mapinduzi ya kiuchumi na kijamii kupitia mitandao ya kijamii, hasa mtandao wa YouTube.

Tulsi ni kijiji chenye nyumba za ghorofa moja na barabara pana za vumbi. Tangi la kuhifadhia maji likitazama mji. Pesa ambazo watu huzipata kupitia YouTube zimebadilisha uchumi wa kijiji, wenyeji wanasema.

Wakazi ambao wameunda chaneli za YouTube na kujipatia mapato ni pamoja na wanawake ambao hapo awali walikuwa na fursa chache za kujiendeleza katika mazingira haya ya mashambani.

Takribani watu 4,000 wanaishi Tulsi, na ripoti zinaonyesha zaidi ya 1,000 hutengeneza maudhui kwa ajili ya YouTube. Ukitembea katika kijiji chenyewe, ni ngumu kupata mtu ambaye hajaonekana katika mojawapo ya video zinazorekodiwa.

Februari 2025 ni kumbukumbu ya miaka 20 ya YouTube. Takribani watu bilioni 2.5 hutumia jukwaa hili, na India ni mojawapo ya soko kubwa la YouTube kufikia sasa.

"Inawaweka watoto mbali na tabia mbaya na uhalifu," anasema Netram Yadav, 49, mkulima huko Tulsi na mmoja wa watu wanaovutiwa na ushiriki wa kijiji hicho katika mitandao ya kijamii.

Pia unaweza kusoma

Mapinduzi kupitia mitandao ya kijamii

rd

Chanzo cha picha, Suhail Bhat

Maelezo ya picha, Wanakijiji huko Tulsi mara nyingi huacha shughuli zao za kila siku kwa muda ili kushiriki katika upigaji video

Mabadiliko katika matumizi ya YouTube huko Tulsi yalianza mwaka 2018, mtengeneza maudhui ya YouTube, Jai Varma mwenye umri wa miaka 32 na rafiki yake Gyanendra Shukla walifungua chaneli ya YouTube inayoitwa Being Chhattisgarhiya.

"Hatukuridhika na maisha yetu ya kawaida, tulitaka kufanya kitu ambacho kingeruhusu ujuzi wetu ueneee," anasema Varma.

Video yao ya tatu, kuhusu wanandoa vijana wakisumbuliwa Siku ya Wapendanao na wanachama wa Bajrang Dal, kikundi cha Wahindu wa mrengo wa kulia, ilikuwa ya kwanza kusambaa kwa kasi.

Ilipata mchanganyiko wa vichekesho na maoni ya kijamii. "Video hiyo ilikuwa ya kuchekesha, lakini pia ilikuwa na ujumbe, na tuliiacha kwa watazamaji kuitafsiri," anasema Varma.

Wawili hao walipata maelfu ya wafuasi katika muda wa miezi kadhaa, idadi ambayo tangu wakati huo imeongezeka hadi watu 125,000 waliojiunga na akaunti yao na idadi watazamaji wa video zao ikizidi milioni 260.

Wasiwasi wa familia zao kuhusu kutumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii, uliisha baada ya pesa kuingia. "Tulikuwa tukipata zaidi ya rupia 30,000 [pauni 278 au $346] kwa mwezi, na tuliweza kuwalipa watu ambao walitusaidia," anasema Shukla.

Hatimaye yeye na Varma waliacha kazi zao na kuingia moja kwa moja kuunda maudhui ya YouTube.

Mafanikio yao yalitoa msukumo kwa wakaazi wengine wa Tulsi. Shukla anasema timu yake iliwalipa waigizaji wao na kutoa mafunzo kwa wengine katika uhariri na uandishi wa skripti. Baadhi ya wanakijiji walitengeneza akaunti zao wenyewe, huku wengine wakiridhika kujitolea.

Video zao zilitosha kuvutia macho ya viongozi wa eneo hilo. Kwa kufurahishwa na mafanikio yao, serikali ya jimbo ilianzisha studio ya kisasa katika kijiji hicho mwaka 2023.

Mafanikio yao

dx

Chanzo cha picha, Suhail Bhat

Maelezo ya picha, Aditya Bhagel (wa pili kutoka kulia) anatoa maelekezo kwa waigizaji na wafanyakazi wake kabla ya kuanza kurekodi

Kati ya mastaa wote wa mitandao ya kijamii waliozaliwa Tulsi, hakuna aliyepanda juu zaidi ya Pinky Sahoo mwenye umri wa miaka 27.

Sahoo alianza kutuma video akicheza kwenye Instagram Reels na video fupi za YouTube (Shorts). Mafanikio yake yalikuja baada ya Being Chhattisgarhiya kuona video zake na kumsajili kwa ajili ya utayarishaji.

"Ilikuwa ndoto iliyotimia," Sahoo anakumbuka. "Walitambua talanta yangu na kuboresha ujuzi wangu."

Kasi hiyo iliendelea huku kazi yake akiwa na Being Chattisgarhiya ikivutia watengenezaji filamu wa eneo hilo. Hatimaye Sahoo akaigiza filamu yake ya kwanza. Tangu wakati huo mwanamke huyo ameonekana katika filamu saba.

fc

Chanzo cha picha, Suhail Bhat

Maelezo ya picha, Video za maisha ya vijijini India zimekusanya watazamaji kutoka kote ulimwenguni

Mkazi wa Tulsi, Aditya Bhagel alikuwa bado chuoni pale alipovutiwa na Varma na Shukla, aliamua kuanzisha chaneli yake mwenyewe. Akaiga mbinu zao, akapata wafuasi zaidi ya 20,000 ndani ya mwaka mmoja na kuanza kupata pesa kutoka YouTube.

Hatimaye, Varma waliamsajili kwa kazi ya kuandika na kuongoza kwenye timu ya Being Chattisgarhiya. "Ilikuwa kama kukutana na watu mashuhuri," anasema Bhagel, akikumbuka mkutano wake wa kwanza na Varma na Shukla.

Mafanikio yake yaliongezeka hadi alipopata jukumu la kuwa mwandishi wa skripti na mkurugenzi msaidizi wa filamu ijayo ya bajeti kubwa inayoitwa Kharun Paar.

Fursa kwa wanawake

d

Chanzo cha picha, Suhail Bhat

Maelezo ya picha, Draupadi Vaishnu, Sarpanch wa zamani wa Tulsi, hutoa eleimu kuhusu umuhimu wa heshima na usawa kwa wanawake nchini India kupitia video zake kwenye YouTube

"Huko Tulsi, YouTube imefungua njia kwa wanawake." Anasema Draupadi Vaishnu, Sarpanch wa zamani, au mkuu wa kijiji cha Tulsi:

"Ni kawaida kwa wanawake kuendeleza [mila potofu], hasa wanavyowatendea mabinti-wakwe zao. Video hizi husaidia kuvunja mila hizo."

Hivi karibuni mzee huyo wa miaka 61 alirikodiwa kwenye video akizungumzia mada hiyo. "Nilifurahi kushiriki kutoa elimu kwa sababu ni muhimu kuwatendea wanawake vyema na kwa usawa."

Kulikuwa na utitiri wa waundaji wa maudhui ya vijijini nchini India wakati wa janga la Covid-19, haswa kwenye TikTok, kabla ya India kupiga marufuku mtandao huo wa kijamii 2020.

Wimbi hilo la awali liliendeshwa na wanaume, anasema Shriram Venkatraman, profesa katika Chuo Kikuu cha Kusini mwa Denmark ambaye anafuatilia athari za mitandao ya kijamii nchini India.

"Lakini kwa sasa kuna wanawake wengi wanaoendesha akaunti zenye wafuasi wengi katika mitandao ya kijamii baada ya janga la corona," anasema Venkatraman, "na hiyo imeunda fursa mpya za kiuchumi."

"Baadhi hata huanzisha biashara zingine kutokana na YouTube kwa kutumia wateja wao na watazamaji wa maudhui kama wateja wao wakuu."

Lakini kwa wengine, pesa sio kichocheo. "Ninapenda kushiriki katika video zinazotolewa na chaneli za kijiji changu, na ninafanya hivyo bila kutarajia malipo," anasema Ramkali Varma mwenye umri wa miaka 56 (hana uhusiano na Jai Varma), ni mama wa nyumbani.